Wednesday, February 22, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI NDOGO YA KAMATI KUU​

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI NDOGO YA KAMATI KUU​


1.0 UTANGULIZI

Kikao cha Kamati Ndogo ya Kamati Kuu cha dharura kilichoketi tarehe 14 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Bahari Beach kilipata nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu matukio mbalimbali yanayoeendelea hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutolewa kwa kauli mbalimbali na viongozi wa kiserikali na ambazo zimeendelea kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa nchi yetu haiendeshwi kwa misingi ya kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni tulizojiwekea kama Taifa .

Aidha Kamati hiyo ilipata muda wa kutafakari kwa kina zaidi juu ya Operesheni UKUTA ambayo tumeendelea kufanikiwa katika kuitekeleza kwa vitendo na pia watanzania wengi zaidi sasa wameona umuhimu wa kuendelea na Operesheni UKUTA kwani Taifa linaelekea kwenye kutumbukia kwenye utawala wa kutokufuata Katiba na Sheria za Nchi (Udikteta kamili).

Mwalimu Nyerere Julai 19, 1967 alisema hivi kuhusu udikteta “Udikteta ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache na wao ndiyo huwa sheria.Anayepinga watakayo,basi huonyeshwa cha mtema kuni”

Kamati hiyo imejiridhisha bila shaka kuwa sasa Chama chetu kinawindwa na watawala pamoja na Rais Mwenyewe na hii ni katika kuelekea kufikia lengo la Rais alilolitangaza alipokuwa Singida mwezi Juni ,2016 ya kuhakikisha kuwa upinzani unakufa ,ifikapo au kabla ya mwaka 2020.

Aidha Kamati hiyo imejiridhisha bila shaka ya kuwa sasa zinatengenezwa chuki za makusudi baina ya vyombo vya dola na wananchi . Hii inatokana na ukweli kuwa Amiri Jeshi Mkuu alisikika akiagiza Polisi wawe na utaratibu unaofanana na Jeshi la Wananchi. Hii ina maana kwamba Polisi lisiwe tena ni jeshi la kulinda wananchi na mali zao bali ni jeshi la kuilinda serikali .

Tumeshaona tayari Polisi wamepiga marufuku (Tamko la Advera –msemaji wa jeshi la Polisi) wananchi kwenda kuwatembelea ndugu , jamaa na marafiki wanapokuwa katika vituo vya polisi bila hata kutaja kifungu cha sheria kinachowapa mamlaka hayo.

2.0 KAMATAKAMATA NA FUNGAFUNGA YA WAPINZANI

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 viongozi na wanachama wa CHADEMA wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kubambikiziwa kwa kisingizio cha uchochezi na mpaka sasa kuna jumla ya wanachama na viongozi 215 ambao wamefunguliwa kesi zaidi ya 78 katika nchi nzima .Wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi . Na wale ambao walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila ya kupewa fursa ya faini.

Hivi sasa umekuwa ni mtindo kwa mahakama kuwakatalia dhamana wanachama wa CHADEMA bila ya sababu za msingi.Pia imekuwa ni mtindo kuwahukumu vifungo bila kuwapa fursa ya kulipa faini.

Tumeamua na tunandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za jinai ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo vilivyotolewa ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za ndani na nje ya nchi kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi wa upinzani kwa kusudi ili kuudhoofisha upinzani.

3.0 VITUKO VYA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KUTANGAZA MAJINA YA WATU HADHARANI KUWA WANAHUSIKA NA DAWA ZA KULEVYA

Chama kinaunga mkono jitihada za dhati za kupambana na madawa ya kulevya nchini, kama sheria na taratibu tulizojiwekea zitafuatwa kikamilifu wakati wa mapambano hayo.

Kamati kuu inalaani kwa nguvu zote kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda) kutangaza majina ya watu mbele ya vyombo vya habari na kuwatuhumu kuwa ama wanahusika katika kusambaza, kuuza au kutumia madawa ya kulevya kwa lengo la kuwachafulia majina, kuwadhalilisha,kuwafedhehesha na kuwaondolea heshima yao kwa umma .Tunalaani kitendo hiki kwa sababu zifuatazo:

i. Mkuu wa Mkoa amekiuka masharti ya Katiba ibara ya 13(6) (b) na (e) ambavyo vinaweka bayana kuwa mtu hatachukuliwa kuwa ametenda kosa la jinai mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kosa hilo na kuwa ni marufuku kwa mtu kuteswa ,kuathibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha

ii. Mkuu wa Mkoa amekiuka kifungu cha 54 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai

iii. Mkuu wa Mkoa hana mamlaka kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayompa kazi na majukumu yake yaani ‘sheria ya Tawala za Mikoa ya 1997’ kuwa ana wajibu wa kutaja majina ya watu anaowatuhumu kuhusika na madawa ya kulevya .

iv. Mkuu wa Mkoa alikiuka ‘sheria ya Kuthibiti na kupambana na dawa za Kulevya,2015’ ambayo haimpi mamlaka ya kutangaza na au kuwataka watu ambao yeye anawatuhumu kujihusisha na usambazaji, uuzaji na au utumiaji wa dawa za kulevya kufika katika vituo vya Polisi .

v. Mkuu wa Mkoa alienda kinyume kabisa na mila na desturi za Kitanzania ,kuwachafulia watu majina na kuwadhalilisha mbele ya jamii huku akijua kuwa hawezi kuwasafisha na wengine ni viongozi wa dini ambao wanaaminiwa na waumini wao .

4.0 HATUA

a. Kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mwenyekiti wetu Taifa Mhe.Freeman Mbowe (MB) ya kumfungulia kesi ya Kikatiba na ya Madai Paulo Makonda katika Mahakama Kuu ya Tanzania na itaungana naye katika kesi hiyo kwa kumpatia mawakili wa Chama .

b. Aidha inatoa wito kwa wale wengine wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa,kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa wafungue mashauri mahakamani , kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine wasifanyiwe uonevu kama huu siku zijazo.

c. Kamati hiyo inawapongeza kwa dhati kabisa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubaliana, kuungana na kuweka itikadi za vyama vyao pembeni wakati wa mjadala wa kulinda hadhi na madaraka ya Bunge. Inatoa rai kuwa waendeleze moyo huohuo kwa siku zijazo kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

5.0 HITIMISHO.

Kamati hiyo inatoa wito ufuatao kwa viongozi, asasi za Serikali, wananchi wazalendo na wanachama wa CHADEMA, kufanya mambo yafuatayo;

1. Viongozi wana wajibu wa kuitetea , kuilinda na kuitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria za Nchi. Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kuwa Rais asiyeweza kuilinda,kuitetea na kuihifadhi Katiba hatufai.

2. Mahakama Itekeleze wajibu wake kwa weledi uliotukuka kuhakikisha kuwa haki sio tu inatendeka bali inaonekana kutendeka bila ya vitisho kwake kutoka kwa mtu yeyote.Iige mfano wa uhuru wa mahakama na weledi wa Majaji wa Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Marekani ambao waliweza kutengua amri batili zilizotolewa na Marais wa nchi zao.

3. Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania watekeleze majukumu yao kwa weledi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.Wasikubali kuwaonea watu kwa misingi ya Vyama ,Itikadi au misimamo yao.Polisi Wajibu wao Kisheria ni kulinda usalama wa raia na mali zao , Jeshi la Wananchi wa Tanzania wajibu wao Kikatiba ni kulinda mipaka ya Nchi.

4. Mawakili wana wajibu mkubwa kuisaidia mahakama kutekeleza majukumu yake kwa weledi kuhakikisha haki inatendeka bila woga ,vitisho au vishawishi .Wasikubali kutishwa na mtu au asasi yeyote katika kuitetea ,kuilinda na kuitekeleza Katiba na Sheria za Nchi.

5. Wasomi na wanataaluma wana wajibu wa kutambua na kuitikia mwito wao wa kutetea ukweli na kulinda haki za jamii hata kama kwa kufanya hivyo kutaathiri maslahi yao binafsi

6. Wanachama tuendelee kudai demokrasia kwa nguvu zote bila woga kwa mujibu wa Katiba na sheria za Nchi.Tushikamane kukikuza Chama kuanzia ngazi ya Misingi hadi Taifa kuendelea na Operesheni UKUTA .

7. Wananchi nchi hii ni yetu sote ni lazima tufaidike nayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi bila vitisho .Tuungane kudai demokrasia na uhuru wa kweli wa kisiasa na kiuchumi. Wasikubali kuyumbishwa na mbinu ovu kama hizi ambazo zimelenga kutupotezea lengo la kuhoji masuala ya msingi kama ufaulu hafifu wa matokeo ya Kidato cha nne Mkoa wa Dar Es Salaam, hali ya chakula nchini (njaa),zilipo milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa , upatikanaji wa Tume huru ya Uchaguzi,Katiba Mpya na hali mbaya ya kiuchumi kwa wananchi .


Mwisho Kamati Ndogo ya Kamati Kuu inawashukuru watanzania wote kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kupambana na udikteta nchini na inawaomba waendelee kuwakumbuka kwa sala/dua viongozi mbalimbali wa Chama waliopo kwenye mateso ya kesi, mahabusu na wengine wanatumikia vifungo kutokana na kuonewa na watawala.​


……………………

Prof. Abdalah Jumbe Safari
Makamu Mwenyekiti Taifa –Bara
16 Februari, 2017​

No comments:

Post a Comment