Thursday, February 2, 2017

KAULI YA TUNDU LISSU KUHUSU HOTUBA YA RAIS KWENYE SHEREHE YA SIKU YA SHERIA

Na TUNDU LISSU

Nimesikiliza sehemu ya hotuba ya Rais Magufuli wakati wa sherehe za Siku ya Sheria leo. Nimemsikiliza aliposema wanaokamatwa na nyara za Serikali au madawa ya kulevya wanastahili kuchukuliwa hatua bila kufuata taratibu za kawaida za kisheria hasa pale wanapokamatwa 'red-handed.' Amesema na mawakili wanaowatetea nao wanastahili kukamatwa na kuwekwa rumande ili na wao 'waisome namba' ili, pengine, waache kuwatetea 'wakosaji' hawa. Wote waliokuwa wanamsikiliza Rais, akiwemo Kaimu Jaji Mkuu na Majaji wenzake wa Rufaa na wa Mahakama Kuu, mawakili na wageni wengine waliokuwapo pale, waliangua kicheko kikubwa. Wanafikiri alichokisema ni cha kuchekesha. It's not funny at all. Jeshi letu la polisi limekubuhu katika kusingizia watu vitu vya uongo.

Kwa polisi wa nchi hii, planting evidence, kuwekea watuhumiwa nyara za serikali au madawa au silaha ili wawakamate na kuwafungulia mashtaka mazito ili kuwakamua watoe pesa, ni kitu cha kawaida sana. Polisi wetu wamekubuhu katika kusachi watu bila kuwa na search warrants na bila kufuata sheria na taratibu za kufanya sachi. Hivi ndivyo wanavyopandikiza ushahidi. Polisi wetu wamekubuhu katika kutesa watuhumiwa ili wakiri makosa ambayo, mara nyingi, hawakuyafanya. Yote haya tunayafahàmu na mawakili, majaji na mahakimu wa nchi hii wanayafahamu sana. Wanakutana nayo kila siku mahakamani. Kauli ya Rais wetu kwamba watuhumiwa hawa washughulikiwe mara moja bila kujali taratibu za kisheria zilizopo ni baraka kwa matendo haya machafu ya jeshi letu la polisi. Ni presidential blessings for state lawlessness na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Ndicho kitakachofuatia bila shaka yoyote. Yamekuwa yanatokea muda wote, sasa yataongezeka kwa sababu yana baraka za Rais.

Kilichonishangaza mimi sio alichosema Magufuli, huyu tumeshamzoea, bali reaction ya waliokuwa wanamsikiliza ambao wanafahamu fika madhara ya kauli hii ya Rais. Kwingineko duniani mawakili wangetoka nje in protest na Rais angeshambuliwa vikali kila mahali kwenye vyombo vya habari, kama tunavyoona yanayomtokea Donald Trump Marekani. Sio Tanzania. Kwetu kila anaona ni kichekesho. Kuhusu mawakili kukamatwa. Miezi kadhaa iliyopita Kamanda wa Polisi Zanzibar Ahmed Msangi, kama sikosei, alitoa kauli ya kuwatisha mawakili wa Zanzibar waliokuwa wanawatetea watuhumiwa wa kesi za kisiasa walizofunguliwa viongozi na wanachama wa CUF huko Zanzibar. Kamanda huyo alisema mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao nao watakamatwa na kuwekwa ndani. Kauli hiyo ilishambuliwa vikali, na kwa usahihi kabisa, na Chama cha Mawakili Zanzibar na wenzao wa TLS. Leo Magufuli ametoa kauli hiyo hiyo, na waliokuwa wanamsikiliza wamechekelea badala ya kutoka nje ya ukumbi in protest!!!! Tusubirie tuone kama TLS watadiriki kutoa kauli ya aina waliyoitoa wakati wa sakata la Zanzibar au wakili mwenzao alipokamatwa Loliondo.

Mimi binafsi nina mashaka makubwa kama watadiriki kufungua mdomo. Katiba yetu inatamka wazi kwamba kila mtuhumiwa anahesabika kuwa hana hatia mpaka mahakama zitakapothibitisha vinginevyo. Rais Magufuli haamini hivyo. Kwake kila mtuhumiwa sio tu ana hatia bali pia hastahili kusikilizwa wala kupata utetezi wa wakili mahakamani. Anachostahili ni adhabu tu, and the bigger the punishment the better. Katiba yetu inasema kila mtuhumiwa ana haki ya 'kusikilizwa kwa ukamilifu.' Haki hii, kama ambavyo mahakama zetu za juu zimesema mara kwa mara, inajumuisha kusikilizwa kupitia kwa wakili. Na juzi Jumanne tumepitisha haraka haraka na kwa mbwembwe nyingi Sheria ya Msaada wa Kisheria. Sheria hiyo inasema kila mtuhumiwa wa kesi ya jinai ana haki ya kupatiwa wakili bila malipo yoyote kama Jaji au hakimu akiona inafaa. Mtendaji Mkuu wa Mahakama, mteule wa Rais, amepewa mamlaka ya kuwalipa mawakili watakaowatetea watuhumiwa hawa. Kwa hiyo fedha za umma zitatumika kuwalipa mawakili watakaowatetea watuhumiwa hawa wa makosa ya jinai. Bila shaka Muswada wa Sheria hii ulipitia kwenye Baraza la Mawaziri kama ilivyo kawaida. Leo Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anatamka hadharani kwamba mawakili watakaowatetea watuhumiwa wanaokutwa na nyara za serikali au madawa ya kulevya nao wakamatwe na kutiwa ndani.

Waziri ambaye juzi alikuwa anashadidia watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria bila malipo anachekelea kauli ya Rais. Majaji na mahakimu watakaoamua watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria nao wanachekelea. Na mawakili ambao wanatakiwa na sheria watoe msaada wa kisheria na ambao watakuwa victims wa kauli ya Magufuli nao wanachekelea. I can only imagine Rais Uhuru Kenyatta angetoa kauli ya aina hii mawakili, wanasiasa, waandishi habari na wananchi wa kawaida wa Kenya wangemfanyaje. Wa kwetu wanachekelea. This happens only in Tanzania.

No comments:

Post a Comment