Thursday, December 15, 2016

LOWASA AWEKEZA IMANI KWA TB JOSHUA,ASEMA CHADEMA ITAONGOZA NCHI UCHAGUZI UJAO

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema ataingia Ikulu baada ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa Serikali ijayo itaongozwa na Chadema.

Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais mwaka jana, ameshaonyesha nia ya kuingia tena kwenye mpambano huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema mkoani Tabora, waziri huyo mkuu wa zamani alisema ana uhakika wa kuingia Ikulu bila ya umwagaji wa damu.

Huku akishangiliwa, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwashukuru wana Tabora na Watanzania kwa ujumla kwa kura walizompa katika uchaguzi mkuu uliopita.

Lowassa aliwaeleza wanachama na viongozi wa chama hicho kuhusu utabiri wa T.B.Joshua na angalizo alilompa.

Alisema muhubiri huyo maarufu barani Afrika anayefanya shughuli zake nchini Nigeria na ambaye alikuja nchini mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, alimpa angalizo kuwa ili washinde ni lazima wawe wamoja, washikamane na kuwa majasiri.

“Najua waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu Joshua ametabiri Serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,” alisema.

Lowassa amekuwa akienda Lagos, Nigeria kuhudhuria ibada za T.B Joshua anayeongoza kanisa la The Synagogue Church of All Nations na ambaye amekuwa akitabiri matukio makubwa kutokea sehemu mbalimbali duniani.

Katika kudhihirisha urafiki wake na T.B Joshua, Lowassa alisema katika mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka, kuwa CCM ilimuita nabii huyo nchini baada ya uchaguzi ili amshawishi akubali matokeo.

Lowassa aliwaambia wanafunzi hao kuwa alimweleza T.B Joshua matukio yote yaliyotokea wakati wa uchaguzi na hivyo kumfanya nabii huyo aamue kutohudhuria sherehe za kuapishwa.

Hata hivyo mwenyewe T.B Joshua hajathibitisha kauli hiyo ya Lowassa. Kuhusu Tabora, Lowassa alisema ni mkoa wa kihistoria na ndio kitovu cha siasa nchini kwa kuwa ndiko kulikoanza vuguvugu la mapambano ya kudai uhuru na kwamba una heshima yake kisiasa.

Aliwataka viongozi na wanachama wa Chadema kuhakikisha wanalinda heshima hiyo kwa kuifanya Chadema kuongoza nchi.

Lowassa, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliwaeleza wanachama na viongozi kuwa ruzuku ni fimbo ya kuwagombanisha wanachama katika vyama vya siasa.

Aliwataka wanachama na viongozi kuhakikisha hawagawanywi na ruzuku na kwamba waulinde Ukawa na wakatae kuvurugwa.

“Vyama vingi nchi za Afrika hugawanywa kwa fedha za Serikali zilizopo madarakani, jambo ambalo sisi tulikatae,” alisema.

Aliwaleza wanachama hao ruzuku inatolewa ili wanachama wabaki wakigombana na kushindwa kufanya mambo ya msingi.

Akiizungumzia elimu, Lowassa alisema CCM inapata ushindi katika maeneo ambayo yapo nyuma kielimu na kuitaja mikoa ya Singida, Mtwara, Lindi, Dodoma na Tabora.

Alieleza kuwa mikoa iliyo nyuma kielimu ndio ngome ya chama tawala na kwamba ndio maana anaposisitiza elimu itolewe bure, anajua anachomaanisha.

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli aliambatana na mjumbe mwingine wa Kamati Kuu ya Chadema, Mwita Waitara, ambaye katika hotuba yake alisisitizia suala la tume huru ya uchaguzi.

Waitara, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ukonga aliwataka wanachama wa Chadema kusimama imara kudai tume huru.
Awali, mratibu wa Chadema wa Kanda ya Magharibi, General Kaduma alisema watu watakaojaribu kuwagawa wanachama, watawekwa pembeni ili wawaache wengine waendelee kuongoza chama.
Alisema madhumuni ya mikutano ya ndani ya chama hicho inayoendelea nchi nzima ni kupanga mambo yanayohusu ujenzi wa chama chao na kuwakumbusha viongozi mambo ya msingi ya chama.

No comments:

Post a Comment