Tuesday, September 13, 2016

Mwenyekiti Taifa wa CHADEMA aelekea Kagera

Mwenyekiti Taifa wa CHADEMA aelekea Kagera



Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari na umma wa Watanzania kwa ujumla kuwa kutokana na madhara makubwa, vikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa makazi ya watu uliosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea juzi Jumamosi, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe amelazimika kukatisha ratiba ya shughuli zingine za kikazi na tayari yuko safarini kuelekea mkoani Kagera.

Mwenyekiti Mbowe anatarajiwa kutua Bukoba mjini majira ya saa 6 mchana, ambapo moja kwa moja akiongozana na viongozi wa Chama na Serikali, aatanzia katika Manispaa ya Bukoba ambapo baada ya kupata taarifa ya kina juu ya athari zilizopo hadi sasa, atapita katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo.

Mojawapo ya maeneo ambayo Mwenyekiti atakwenda kujionea athari kubwa zilizotokea ni pamoja na Shule ya Sekondari Ihungo ambayo Mwenyekiti Mbowe alisoma kidato cha 5 na 6. Hadi sasa inaelezwa kuwa shule hiyo ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa sana na janga hilo la juzi.

Mwenyekiti atafika kuwapatia pole na kuwafariji waathirika wa tetemeko, waliofiwa, waliojeruhiwa na wale ambao wamelazimika kujihifadhi katika viwanja vya mpira baada ya makazi yao kuharibiwa vibaya.

Chama kinaendelea kutoa pole kwa waathirika wote wa tetemeko hilo huku pia kikitoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuguswa na kuwa pamoja na wenzetu waliokumbwa na maafa hayo makubwa.

Imetolewa Jumatatu, Septemba 12, 2016 na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment