Friday, August 26, 2016

Serikali ya CCM isipoacha tabia hii ya kuona Wapinzani ni Magaidi itaangamiza hili taifa

Jeshi la Polisi wilayani Mbozi leo limemkamata Afisa wa Teknolojia ya Habari wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa) Mdude Nyagali kwa madai ya kuandika uchochezi katika ukurasa wake wa Facebook, kuhusiana na tukio la kuuawa kwa askari polisi wanne huko Mbande jijini Dar.

Mbali ya kumkamata Polisi wamempiga sana na kumvunja miguu yote miwili. Licha ya kumvunja miguu Polisi wamekataa kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu. Viongozi wa Chadema waliokusanyika katika kituo cha Polisi Vwawa aliposhikiliwa Afisa huyo wamekataliwa kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu.

Tangu asubuhi Polisi walipomkamata, wamekua wakimpiga na kumshinikiza kutoa maelezo juu ya taarifa za uchochezi anazodaiwa kuandika. Lakini Ndugu Mdude amekataa kufanya hivyo kwa madai kuwa hawezi kutoa maelezo yoyote hadi Mwanasheria wake afike. Kwa sasa Mwanasheria wa Chadema kanda ya Kusini anaelekea mjini Vwawa akitokea Mbeya ili kumsaidia Mdude kutoa maelezo.

Licha ya kumvuja miguu Polisi pia wamempiga sehemu nyingine za mwili na kumsababishia majeraha kadhaa, pia wamemchania nguo zake kitendo ambacho ni cha udhalilishaji. 


Mdude Nyagali


#MyTake:
Nalaani vikali kitendo alichofanyiwa ndugu Mdude. Sio kwa sababu ni kada mwenzangu wa Chadema, ila ni kwa sababu nae ni binadamu. Ana haki ya kuheshimiwa na kulindiwa utu wake hata kama angekua CCM. Ukatili aliofanyiwa Mdude unapaswa kupingwa na kulaaniwa na kila binadamu mwenye utashi na akili timamu.

Pia nashauri Polisi waliohusika na ukatili huu wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kisha kushtakiwa. Hivi Polisi hawajui mtuhumiwa ana haki? Hivi Polisi hawajui maana ya "presumption of inocense" kwa mtuhumiwa? Kuna sababu gani ya kumpiga mtuhumiwa ambaye hajaonesha reaction yoyote?

Taarifa niliyopata ni kuwa Polisi walipofika nyumbani kwa Mdude walianza kumpiga kabla hata ya kumfikisha kituoni. Na walipomfikisha kituoni wakashirikiana kumpiga na hatimaye kumvunja miguu yote miwili. Uongozi wa CHADEMA wilayani Mbozi umeomba kumpeleka hospitali lakini umekataliwa. Pia baadhi ya viongozi wamepeleka magongo ktk kituo cha Polisi Vwawa angalau yamsaidie kusimama lakini polisi wamekataa kupokea magongo hayo.

Natoa wito wabunge wote wa Chadema mkoa wa Mbeya waungane kupinga unyama huu aliofanyiwa mwenzetu. Joseph Mbilinyi, Sophia Hebron, Silinde Ernest David, Pascal Haonga na Frank Mwakajoka najua mnanisoma hapa. Tafadhali chukueni hatua ya haraka dhidi ya ukatili huu. Hatuwezi kuendelea kuvumilia watu wetu wakifanyiwa uhuni wa kiwango hiki.

Ameuawa Kamanda Mawazo tukakaa kimya, wamekamatwa makamanda wengi na kubambikiziwa kesi tupo kimya, sasa wameanza kutuvunja miguu na kutufanyia unyama na ukatili usiovumilika. Hii si sawa hata kidogo. Tukinyamaza hata Mungu atatuhesabia dhambi.

Polisi wanapaswa kuheshimu sheria. Kama hawataki kuheshimu sheria kwa hiyari yao, tutawalazimisha kuziheshimu. Kazi ya polisi si kupiga na kuua. Kazi ya Polisi ni kulinda usalama wa raia na kuzuia uhalifu. Polisi haruhusiwi kutumia nguvu bila sababu. Hata ikifikia mahali pa kutumia nguvu sheria inasema iwe nguvu ya kawaida (reasonable force).

Lakini nguvu iliyotumika kwa Mdude sio reasonable. Wameenda nyumbani kwa Mdude wakiwa na silaha, wakamkuta hana hata fimbo lakini bado wakampiga. Huu ni upumbavu. Kwanini mtumie nguvu mahali pasipohitaji nguvu? Mlipaswa kumkamata na kumfikisha kituoni akiwa salama, kisha mumfungulie mashtaka mnayoona yanamfaa then mumfikishe majakamani.

Kwanini mumpige? Kwanini mnahukumu kabla ya mahakama? Kuanzia lini kazi ya Jeshi la Polisi imekuwa ni kuhukumu? Kwanini mnatumia mabavu kutesa raia? Kwanini hayo mabavu msiyatumie kupambana na wahalifu? Ona sasa mmemsababishia kamanda wetu ulemavu wa kudumu.

Hata kama atapona na kutembea tena lakini Mdude atakuwa mlemavu wa miguu kwa maisha yake yote. Kwahiyo hata ikitokea Mahakama ikimkuta hana hatia tayari atakuwa mlemavu. Hii si sawa kabisa....

Seriakali ya CCM isipoacha upuuzi huu wa kuona wapinzani ni magaidi itaangamiza hili taifa. Narudia kusema serikali ya CCM na vyombo vyenu vya dola acheni upumbavu. Takwimu za Umoja wa mataifa za mwaka huu zimeonesha wastani wa polisi kwa raia nchini ni 1:15000 yani askari mmoja anahudumia raia 15000. Hivi raia wakiamua kureact ni polisi gani atapona. Ni askari gani anaweza kusurvive kwenye nguvu ya raia 15000?? Hata awe na silaha za kivita hawezi kupona? Kwahiyo acheni ujinga. Hii nchi ni yetu sote. Msijione nyie mna haki kuliko wengine. Tumieni sheria kutekeleza kazi yenu sio kufanya kazi kwa mihemko ya kisiasa.!

Malisa G.J

No comments:

Post a Comment