Saturday, August 20, 2016

Kibatala aibwaga Serikali

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa uamuzi wa hoja zilizokuwa zikibishaniwa na mawakili wa pande mbili katika kesi ya uchochezi inayomkabili Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), anaandika Faki Sosi.

Hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza, ya kwamba wakili Peter Kibatala hana uhalali wa kumtetea Lissu katika kesi hiyo kutokana na kuwa ni mmoja wa mashahidi wa upande wa Jamuhuri, ilikuwa ikitolewa uamuzi.

Cyprian Mkeha, Hakimu Mfawidhi katika mahakama hiyo ametoa uamuzi wa shauri hilo kwa kutupilia mbali hoja za upande wa mashitaka.

Hakimu Mkeha, amesema kuwa, hakuna sheria yoyote inayomzuia Kibatala kumtetea mteja wake kama upande wa mashitaka ulivyodai na hivyo ataendelea kumtetea Lissu.

Baada ya uamuzi huo kutolewa, kesi hiyo itatajwa tena tarehe 19 Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment