Saturday, July 23, 2016

Chadema: Tunailenga 2020

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza mkakati wa kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, anaandika Pendo Omary.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), kilichomalizika leo jijini Dar es Salaam Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho amesema, ifikapo mwaka 2018 chaguzi zote ndani ya chama zinapaswa kuwa zimekamilika ili kujipanga na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Ili tuweze kushinda ni lazima kutambua na kuhamasisha watu makini wenye sifa stahili za kushika nafasi mbalimbali za uongozi na pia kujiunga na chama (kwa wasio wanachama ).

“Lazima mtambue mapema ukubwa wa kazi hii na kuanza kujipanga kuikamilisha kwa ufanisi; hili ndilo jukumu la kwanza ninalotoa kwa baraza la vijana,” amesema Dk. Mashinji.

Mashinji amesema, baraza hilo linapaswa kutambua uongozi katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa ni jukumu la vijana katika kujenga uzoefu na uelewa wa kiuongozi ndani ya taifa.

“Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, tunatarajia kuwa na Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na rais kwa bara. Kwa Zanzibar kutakuwa pia na uchaguzi wa wawakilishi na rais wa Zanzibar.

“Kama maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu kwa mwaka 2016, kila ngazi lazima itambue nafasi ambazo zitagombewa kwenye eneo lake kwenye uchaguzi mkuu.

“Kwa kuwa vijana watakuwa wameshikilia uongozi wa serikali za mitaa, hivyo ni amani yangu kuwa nguvu kubwa itakwenda kwenye kushinda nafasi ya udiwani; hili ni jukumu la tatu na la mwisho ninalowatuma kwa kipindi hiki,” amesema Dk. Mashinji.

Mwanahalisi online

No comments:

Post a Comment