Monday, June 20, 2016

Katibu mkuu CHADEMA Dkt.Vicent Mashinji kuhudhuria kongamano Ujerumani

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Katibu Mkuu wa Chama, Dkt. Vincent Mashinji ni miongoni mwa wajumbe 23 kutoka nchi 20, duniani walioalikwa kuhudhuria kongamano litakalojadili, pamoja na masuala mengine, umuhimu wa sauti za wananchi kupitia vyombo vya uwakilishi kama bunge, katika maendeleo ya taifa na watu wake.

Kongamano hilo litakaloanza Juni 20-25, mwaka huu nchini Ujerumani, pia litajadili mikakati ya kampeni na kushinda uchaguzi, hususan kwenye mazingira yenye changamoto mbalimbali za kisiasa huku pia wakijifunza umuhimu na nafasi ya Serikali za Mitaa katika maendeleo ya wananchi.

Kupitia kongamano hilo, Katibu Mkuu Dkt. Mashinji pamoja na washiriki wengine watajadili kwa kina na kubadilishana uzoefu wa ushindani wa siasa kutoka maeneo mbalimbali, huku pia wakijifunza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mawasiliano kupambana na changamoto za kisiasa, hasa katika nchi zinazoendelea.

Mada zingine katika kongamano hilo zitahusu; mawasiliano kati ya serikali na wananchi, kuwasaidia vijana kutambua umuhimu wa siasa na kushiriki. Aidha, watajifunza mafanikio ya chama tawala cha Ujerumani, CDU, namna ambavyo kwa miaka 70 sasa, mipango, mikakati na sera zake zimesaidia kuboresha maisha ya Wajerumani kiasi cha taifa hilo kuongoza kwa maendeleo barani Ulaya.

Mbali na Katibu Mkuu Dkt. Mashinji kutoka Tanzania, kongamano hilo la majira ya joto, litawakutanisha washiriki kutoka nchi za Ufaransa, India, Ujerumani, Ghana, Philippines, Mexico, Mongolia, Argentina, Ukraine, Poland, Bolivia, Cambodia, Syria, Tunisia, Uganda, Kurdistan, Venezuela, Hoduras na Ugiriki.

Imetolewa leo Jumamosi, Juni 18, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment