Sunday, May 15, 2016

SUMAYE ATEULIWA KUWA MJUMBE WA KAMATI KUU CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemteua Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu.

Uamuzi huo unatokana na kikao cha Kamati Kuu kilichoketi mjini hapa kwa siku mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu Zazinzar, Salum Mwalimu alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe ana mamlaka ya kuteua majina sita ya wajumbe wateule.

Alisema katika kikao hicho mambo mengi yamezungumzwa lakini pia kuna mambo ya kimkakati hasa katika kuelekea kumaliza mwaka huu na kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mwalimu alisema katiba yao ya mwaka 2006, inazungumzia wajumbe wateule wasiozidi sita ambao watapendekezwa na mwenyekiti wa taifa kwa kushauriana na katibu mkuu na kuridhiwa na vikao.

Alisema Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho ametumia kipengele hicho kupendekeza jina la Sumaye kuwa mjumbe wa kamati kuu na jina hilo liliungwa mkono na kikao na kuafikiwa na kamati kuu.

No comments:

Post a Comment