Wednesday, May 11, 2016

MEYA WA DAR ATAKA TAARIFA ZA MAPATO KUTOKA TRA ILI AJIRIDHISHE



Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji kumwandikia Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuomba taarifa za mapato halisi za benki zilizopo Dar es Salaam ili kujiridhisha na kiwango kinachotolewa na benki hizo wakati wa kulipa ushuru wa huduma za Jiji (City Service Levy).
Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mhe. Isaya Mwita amesema kuwa kutokana na kutoridhishwa na taarifa ya mapato iliyotolewa katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Jiji hilo,lililofanyika Mei 02 mwaka huu ikionesha mapato ni madogo kulingana na wingi wa vyanzo vya mapato vilivyopo.

“Kwa mujibu wa taarifa tulizopokea kuhusu vyanzo vya mapato vya Halmashauri ya Jiji haviendani na vyanzo vilivyopo hasa ushuru utokanao na huduma za Jiji zinazotolewa kwa mabenki mbalimbali yaliyopo ndani ya Halmashauri,” Alisema Mwita.

Mstahiki Mwita ameongeza kuwa ingawa Halmashauri inapata taarifa za benki kutoka Benki Kuu (BOT) lakini kumekuwa na mkanganyiko wa uwiano wa makusanyo ya mapato na idadi ya benki zilizopo zinazopatiwa huduma za Jiji hivyo ameagiza kupata ufafanuzi kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ili kujiridhisha.

Aidha Mstahiki Meya amempa Mkurugenzi wa jiji hilo, wiki moja kuwasilisha taarifa yenye orodha ya idadi ya benki zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam na zinazotakiwa kulipa ushuru.

Kwa mujibu wa sheria za huduma ya Jiji watumiaji wote wa huduma hizo wanatakiwa kulipia ushuru wa huduma hizo kwa wakati na kuwataka kulipa ushuru uliopo kwani sio majadiliano bali ni sheria na wanatakiwa wazifate kwa maendeleo yao na ya Jiji.
  • Raymond Mushumbusi MAELEZO

No comments:

Post a Comment