Wednesday, May 18, 2016

BAVICHA wamvaa Rais Magufuli, Jaji Mkuu

BARAZA la Vijana wa Chadema (BAVICHA) limemtaka Rais John Magufuli kuacha kuingilia bunge na kuamuru nini kijadiliwe, anaandika Pendo Omary.

Limefikia hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Mussa Azzan Zungu, Mwenyekiti wa Bunge kuagiza kuondolewa baadhi ya vipengele katika Hotuba ya Godbless Lema ambaye ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Vipengele hivyo vilihusu; mauaji ya viongozi wa kisiasa, mkataba tata wa Lugumi, uuzwaji wa nyumba za serikali, Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, sakata la vitambulisho vya taifa (Nida), mwenendo wa rais, kashfa ya ununuzi wa rada na bunge kulinda walarushwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari leo kwenye Makao Makuu ya chama jijini Dar es Salaam, Julius Mwita, Katibu Mkuu BAVICHA amesema, “vipengele katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – Wizara ya Mambo ya Ndani vililazimika kuondolewa bungeni kwa sababu ya Rais John Magufuli.

“Tunashuhudia Rais Magufuli ndio anaongoza bunge kutoka Ikulu. Baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapigiwa simu na kutishwa akiwemo Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera.

“Hata spika na naibu spika wanapata maelekezo ya kuendesha bunge kutoka kwa rais. Hotuba hii tutaendelea kuisambaza hadi kila mtu aisome,” amesema Mwita.

Mwita amesema, kutajwa kwa Charles Kitwanga, Waziri wa Mambo ya Ndani kudaiwa kuwa mbia wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited, iliyoingia mkataba tata na Jeshi la Polisi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. 35 Bilioni, ni sababu tosha ya waziri huyo kuwajibika au Rais Magufuli kutengua uteuzi wake ili kuipa uhuru Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuchunguza mkataba huo.

“Tunajua wazi bunge lingekubali mkataba wa Lugumi ujadiliwe kungemuingiza Kitwanga kwenye mgogoro. Rais Magufuli ni swahiba wa Kitwanga. Jipu la Lugumi limeonekana kuwa mwiba. Tunamtaka Rais Magufuli achukue hatua,” amesema Mwita.

Aidha, Mwita amemtaka Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu kufuta kauli ya kusifia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 aliyoitoa hivi karibuni nchini Uingereza alipokuwa akizungumza na Watanzania waishio huko kuhusu faida na hasara za sheria hiyo.

“Kazi ya jaji yoyote sio kusifu sheria. Anapaswa kutafsiri sheria kwa msingi wa Katiba. Tunamtaka Jaji Mkuu aondoe tamko hilo haraka. Litasababisha majaji wengine kushidwa kutafsiri sheria hiyo la sivyo tutaitisha “petition” nchi nzima kupinga suala hili. Sisi vijana ndio tunaoumia na sheria hii kuliko makundi mengine,” amesema Mwita.

Katika mkutano huo Mwita aliongozana na Emmanuel Masonga, Mwenyekiti BAVICHA Mkoa wa Njombe na Edward Simbeye, Mwenezi BAVICHA.

No comments:

Post a Comment