Tuesday, May 26, 2015

Dk. Slaa ataka wajawazito, wagonjwa wapewe kipaumbele uandikishaji BVR.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa (pichani), amewataka waandikishaji na wasimamizi wa uandikishaji wa wananchi kielektroniki katika daftari la kudumu la wapiga kura (BVR), kutoa kipaumbele kwa kina mama wajawazito, wazee, wagonjwa na walemavu, ili waweze kujiandikisha bila kupata madhara.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Hamugembe jana baada ya kuzunguka kwenye baadhi ya vituo vya uandikishaji, Dk. Slaa alisema kuwa kitendo alichokutana nacho katika manispaa ya Bukoba cha kukuta mama mjamzito amezimia kutokana na kukaa kwa muda mrefu katika mstari bila kuandikishwa, hajafurahishwa nacho.

“Kama waandikishaji na wasimamizi wa zoezi hili hawafahamu vizuri sheria ya uchaguzi, basi waitafute waisome ili waelewe kuwa makundi haya ya watu hayapaswi kukaa katika mistari muda mrefu, badala yake inabidi wanapofika wahudumiwe na kuondoka,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alimwagiza mwenyekiti wa Chadema Bukoba mjini, Victor Sherejey, kufuatilia katika vituo vyote na kuhakikisha kasoro zilizobainika zinafanyiwa kazi, ikiwamo ya makundi hayo ya watu kuandikishwa bila kusumbuliwa.
Alisema kuwa kila mwananchi mwenye sifa bila kujali hali aliyonayo anapaswa kuandikishwa na kuwa hiki ni kipindi kigumu kuliko vipindi vyote maana uandikishaji ndiyo mwanzo wa kupiga kura, ambaye hatajiandikisha hawezi kulalamika baadaye dhidi ya viongozi wasiofaa watakaochaguliwa.

Aidha Dk. Slaa alizungumzia sheria inayolenga kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kuwa kitendo cha serikali kuandaa kupeleka bungeni muswada wa sheria ya habari kwa hati ya dharura, kuzifunga redio na vyombo vingine, zisitangaze matokeo ya uchaguzi, ili serikali iliyoko madarakani iweze kufanikisha azma yake ya kuiba kura.

“Serikali ina maana gani kuzitaka redio binafsi zijiunge na redio ya taifa kila ifikapo saa mbili, muda huo watu ndipo wanakuwa wametoka kuhangaika na shughuli za hapa na pale wanataka kutulia kusikiliza taarifa za ukweli kutoka vyombo mbalimbali, leo hii serikali inasema redio zote zijiunge na redio ya taifa, huu ni ukandamizaji wa vyombo vya habari,” alisema.

Aliitaka serikali kutowafunga midomo waandishi wa habari hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, maana wananchi wa Tanzania wana haki ya kupata habari sahihi na kwa wakati wanaotaka.

No comments:

Post a Comment