Friday, April 17, 2015

Mbowe: Serikali isithubutu kuahirisha Uchaguzi Mkuu.



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitakubaliana na maamuzi yoyote ya serikali kuahirisha Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, kwa kisingizio cha kuchelewa kukamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alitoa angalizo hilo jana, wakati wa ufunguzi wa programu ya mafunzo itakayofanyika nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Alisema serikali isithubutu kutumia urahisi iliyoupata kuahirisha kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na kutaka kufanya hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ambao unafahamika kikatiba.

“Tarehe ya Uchaguzi Mkuu ilijulikana tangu mwaka 2010 kuwa ni Jumapili ya mwisho ya Oktoba…uandikishaji hadi leo haujamalizika kwenye mkoa mmoja, kuna miezi minne kufika siku ya kuanza kampeni, tunajiuliza ndani ya siku hizo itaweza kuandikisha nchi nzima?” alihoji.

Alisema Chadema imejipanga kuwa kampeni za uchaguzi huo zitakazoanza Agosti 15, mwaka huu ambazo zitatudumu kwa siku 72.

Uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), ulianza mkoani Njombe na Februari 23, mwaka huu na utakamilika kesho.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepokea vifaa (BVR Kits) 498 huku ikiendelea kusubiri vifaa vingine.

Nec ilitangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa iliyotakiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuchelewa uboreshaji wa daftari hilo na kwamba itatangazwa tena baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).

Aidha, Tume hiyo imesema hadi Julai 30, mwaka huu, itakuwa imekamilisha uandikishaji wapigakura kwa mfumo wa BVR na kwa sasa wataanza kwenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Iringa.

USHIRIKIANO IMARA
Mbowe alisema matarajio ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kugombana na ushirika wao kuparaganyika, na kwamba jambo hilo halitawezekana kwa kuwa wamejipanga kikamilifu.

Alisema anatambua majaribu na changamoto za ushirika wowote duniani, hivyo pamoja na changamoto zinazojitokeza kwenye Ukawa, lakini watazishinda na kusonga mbele kwa kushika dola Oktoba, mwaka huu.

“Vikao vya Ukawa vinaendelea vizuri na makubaliano yetu ni yale yale kuwa kila kata, jimbo na rais kutakuwa na mgombea ambaye atapitishwa na Ukawa,” alisema na kuongeza:

“Leo kuna watangaza nia kuliko nafasi za uongozi, sisi Ukawa tunasema watakaopata watapata kwa misingi ya haki na usawa na siyo dhuluma, watakaoshindwa ubunge na udiwani wasiache kuunga mkono wagombea kwa kuwa serikali itakayoundwa itahitaji viongozi wengi ndani ya serikali ya shirikisho,” alisema.

Alisema Dar es Salaam ina dhamana kubwa kwa kuwa katika kushika dola ni lazima kujihakikishia ushindi wa majimbo nane ya mkoa huo.

Alisema walichogundua Ukawa ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2010, Chadema na CUF waligawana kura katika majimbo ya Temeke na Kinondoni na kwamba hawatakubali kuendelea kugawana katika maeneo mbalimbali nchini bali kuwa wamoja.

“Hatufanyi mtihani wa mzaha bali ni wenye kusudio la uhakika tunashika dola…tunatambua kuwa kila chama kina nguvu kwa upande wake ndiyo maana tumejenga ushirikiano kwa matokeo mema ya nchi,” alisema.

Ukawa ni Muungano wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ambavyo vilianzisha umoja huo wakati wa Bunge Maalum la Katiba.

MAANDALIZI YA VIONGOZI
Mbowe alisema viongozi hawazuki bali huandaliwa ndiyo maana Chadema imeanza mpango wa mafunzo kwa viongozi wake nchi nzima na wameanzia na Dar es Salaam, kwa kuwa ina idadi kubwa ya wapiga kura kuliko mikoa yote nchini.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema maandalizi ya viongozi 2 2,4287 yatafanyika katika kanda 10, majimbo 242, kata 4,852, matawi 22,749, misingi 64,803 ya kichama.

Alisema viongozi hao watafundishwa namna ya kutekeleza wajibu wao na kuimarisha wagombea ili wawe wagombea wazuri na kunadi sera zao.

Alisema Dar es Salaam ina majimbo sita kati yake la Kigamboni ndilo lenye wapiga kura wengi ikifuatiwa na mengine ya jiji hilo na kwamba ni kitovu cha mambo yote ikiwamo makao makuu ya nchi na vyombo vyote vya habari.

Alisema dhamana kubwa ya kushinda inategemea Dar es Salaam kwa kuwa kura zake ndizo zitakazoamua nani ataongoza nchi.

Kwa mujibu ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012 na zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dar es Salaam ina wapiga kura 2,932,930.

JOHN MNYIKA
Awali, Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika, alisema wakati anaingia jimbo la Kinondoni, Manispaa ya Kinondoni mwaka 2010, makusanyo ya ndani yalikuwa Sh. bilioni saba, lakini kwa sasa ni Sh. bilioni 35 huku ya Serikali Kuu yalikuwa ni Sh. bilioni 87 na ya sasa Sh. bilioni 84.

Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bara, alisema zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya nchi yanakusanywa Dar es Salaam, hivyo Jiji hilo lina umuhimu mkubwa katika ushindi wa nafasi zote.

SALUM MWALIMU
Naye, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salmu Mwalimu, alisema kutakuwa na timu tatu za kuzunguka nchi nzima kufanya mafunzo hayo zitakazoongozwa na makatibu hao na wata
anza kesho.

No comments:

Post a Comment