Wednesday, March 25, 2015

Muswada wa Baraza la Vijana wamkuna Mnyika.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (pichani), amesema muswada binafsi wa Baraza la Vijana la Taifa unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni Machi 31, mwaka huu utaandika historia mpya kwa vijana.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnyika alisema muswada huo utasomwa kwa mara ya pili baada ya ule wa kwanza uliosomwa katika Bunge la 14 Desemba 21 mwaka 2013.

“Baraza la Vijana la Taifa pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana wa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa,” alisema Mnyika.

Pia alisema, baraza hilo litafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana ikiwamo ajira, elimu na sekta nyingine katika Halmashauri, Serikali Kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo.

“Muswada huo utawezeshwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kulipa jukumu Baraza la Vijana kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla,” alisema.

Mnyika alieleza kuwa Kujadiliwa kwa muswada huo ni hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.

“Natambua mchango wa vijana na taasisi zote za vijana mlioshiriki katika maandalizi ya muswada huu, unaitwa binafsi kwa sababu tu ndio neno linalopaswa kutumika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, lakini ukweli ni kwamba huu ni muswada wenu, mimi ni mwakilishi.”

No comments:

Post a Comment