Saturday, March 28, 2015

Mbowe: Kila chama Ukawa ruksa kuandaa wagombea

Zanzibar. 
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema kila chama ndani ya umoja huo kiko huru kutoa fomu na kuandaa wanachama wake watakaoshindanishwa katika mchakato wa kuwapata wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Tamko hilo lilitolewa na viongozi wakuu wa Ukawa baada ya kumalizika kwa kikao cha siku mbili kilichofanyika Shangani, Zanzibar kujadili hali ya kisiasa na utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema wagombea wa umoja huo watapatikana kwa kuzingatia sifa na uwezo wa kila mmoja na nia ya kweli ya kuleta mabadiliko katika nchi.

“Hakuna chama kinachozuiwa kutoa fomu kutafuta wagombea katika mchakato wa ndani wa chama kabla ya Ukawa kufanya uteuzi wa mwisho,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.


Kuhusu mvutano
Kauli ya Mbowe inakuja wakati kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wanachama na wajumbe wa kamati ya ufundi ya Ukawa kutokana na mvutano wa kila chama kutaka majimbo fulani ambako kila kimoja kinadhani kinakubalika.

Hata hivyo, Mbowe alisema Ukawa inaendelea kuimarika tangu kuasisiwa kwake na hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

“Hakuna mushkeli, uhusiano wetu Ukawa unaendelea kuimarika na tutahakikisha tunasimamisha mgombea mwenye sifa na uwezo wa kutuletea ushindi, hatutagubikwa na masilahi ya vyama, tunataka masilahi ya Ukawa kwanza vyama baadaye.

“Ni ndoto Ukawa kumeguka kwa sababu tumetambua umoja ni nguvu na wenzetu wanasubiri kuona tunameguka,” alisema Mbowe katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.


Gharama za uchaguzi
Alipoulizwa kuhusu gharama za uchaguzi ndani ya Ukawa, Mbowe alisema ni mapema kueleza hilo lakini hawatarajii kumwaga fedha kama wanavyofanya baadhi ya wagombea wa chama tawala katika kutafuta nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo urais wa Muungano... “Ukawa tunajiamini, tuna uwezo wa kushinda dola.”

Awali, Mwenyekiti wa CUF ambaye pia mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kikao hicho kimepata mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa wagombea wa Ukawa watatangazwa baada ya kukamilika mchakato ndani wa vyama.

Alisema kwa mwelekeo wa kisiasa baada ya kufanya tathmini, Ukawa ina nafasi kubwa ya kuingia Ikulu ya Muungano na Zanzibar mwaka huu kutokana na CCM kushindwa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Alisema lengo kubwa la Ukawa ni kuwa na Tanzania mpya yenye maendeleo na sera ya maisha bora kwa Watanzania wote na kuwataka wananchi kuwa tayari kuyapokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake si msindikizaji katika Ukawa na nia yake ni kuona mabadiliko ya kiutawala yanatokea. Aliwataka Watanzania kuwa tayari kufanya uamuzi mgumu.

“Tayari nimeota ndoto Ukawa wanakamata madaraka ya nchi mwaka huu,” alisema Makaidi.


Katiba mpya
Akizungumzia Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa, Mbowe alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haiwezi kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja na kutaka Kura ya Maoni isitishwe kwa sababu muda wa maandalizi ni mdogo na imeshindwa kuandikisha wapiga kura kutokana na ukosefu wa vifaa.

Alisema Serikali kuendelea kulazimisha Kura ya Maoni wakati matayarisho ni mabovu kutasababisha vurugu.

No comments:

Post a Comment