Thursday, October 30, 2014

Msigwa: Waliojitangaza kuwania urais hawana dira

Baada ya makada mbalimbali wa CCM kutangaza nia ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anasema bado hajaona mtu mwenye sifa ya kupewa nafasi hiyo kubwa nchini miongoni mwa waliojitokeza.
Hadi sasa ni makada wa CCM pekee waliotangaza nia hiyo ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete, wakati vyama vya upinzani vimeingia makubaliano ya kumteua mgombea mmoja kupambana na chama hicho tawala.
Pamoja na wanasiasa wazito wa CCM kutangaza nia ya kugombea urais na baadhi kuanza harakati kabla ya kutangaza, Mchungaji Msigwa anasema wote waliojitokeza hawana dira ya kuipeleka nchi sehemu fulani kutoka hapa ilipo na hivyo hawastahili kupewa nafasi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa na kijamii, Msigwa alisema kujitangaza kwao siyo tatizo, lakini haoni kama kuna mtu mwenye sifa za urais. “Ukimuuliza kila mmoja kwa waliojitangaza kwamba ana vision (dira) gani kwa ajili ya nchi katika miaka mitano ijayo, wengi watatoa ahadi badala ya kueleza ataifikisha nchi wapi katika muda huo,” alisema mchungaji huyo bila ya kutaja majina ya waliojitokeza.
“Wengi kati ya hawa wanaojitangaza wanataka power (madaraka) ya kulinda status quo (nafasi zao), lakini nakuhakikishia hawana ‘vision’. Wanatumia hela zao kununua madaraka.”
Alisema hata siku moja mti wa mwembe haujawahi kumwita mtu akatungue maembe, bali msimu ukifika watu hufuata mti na kutungua maembe, akimaanisha wanaojitangaza sasa hawajafuatwa na mtu wajitangaze. “Tunahitaji mtu mwenye dira nzuri na si watu ambao watatupa ahadi ambazo hazitekelezeki,” aliongeza mchungaji huyo wa Iringa Vineyard Church na ambaye pia ni mratibu wa taifa wa kanisa hilo.
Pia, Mchungaji Msigwa alisema ni wapinzani pekee ambao wana mtu ambaye ana dira na ambaye wakati ukifika atajitokeza kutangaza kuwania kuingia Ikulu.
“Katika Ukawa viongozi wetu wakiafikiana na tukapata mtu mwenye maono ambaye ana anakubalika pia anaweza kupambana na mambo, tutafanikiwa,” alisema.
Akizungumzia makubaliano ya vyama vya upinzani kusimamisha mgombea atakayeungwa mkono na wote katika ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa alisema, “Kuna tofauti kati ya mwanasiasa na kiongozi. Mwanasiasa ni mtu anayependa kufanya mambo mazuri, lakini kiongozi ni mtu anayefanya mambo sahihi,” aliongeza:
“Mtu anayefanya jambo sahihi mara nyingi anafanya kwa kuwa jambo hilo linakuwa linaumiza, lakini mtu anayefanya mambo mazuri siku zote anafurahia.
“Siasa za siku hizi zimebadilika, hivyo mtu anayezifanya lazima ajue kwamba kuwa mwanasiasa na kuwa kiongozi ni vitu viwili tofauti.”
Hivyo alisema ni muhimu kwa wananchi kuwachunguza hao wanaojitangaza kuwania urais na kuzijua tabia zao kuanzia sasa. “Ukichagua mwizi, lazima atakwenda kuiba kwa sababu ndiyo tabia yake, hivyo ni lazima tuwachunguze, tuwajue ili tusije kuchagua watu wenye hulka ya wizi,” alisisitiza na kuongeza: “Tuwachunguze hawa watu na tusikurupuke.”

Vita na CCM Iringa Mjini
Akizungumzia kauli ya viongozi wa CCM kwamba amekodishwa kiti cha Jimbo la Iringa Mjini, Msigwa alisema: “Lugha kwamba wamenikodisha jimbo ni ya kihuni na ni ya kupuuza. Wanavunja Katiba kwa kuwa hakuna sehemu iliyosema kwamba jimbo ni mali ya CCM.”
Alisema ubunge wake hauna tofauti na wabunge wengine wa majimbo kama ilivyo kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta na kwamba wananchi wa Iringa Mjini ndiyo wanaamua nani anakuwa mbunge wao na si CCM.
“Tukiitisha uchaguzi leo, hata CCM walete mgombea gani pale Iringa Mjini, nitamwacha mbali sana. Nitamwacha kwa asilimia 90 kwa kuwa wamepoteana katika jimbo kiasi kwamba wako watu 15 wanaolitaka,” alisema huku akicheka.
Alisema CCM hawaachi visingizio kwa kuwa sehemu zote Chadema iliposhinda wamekuwa wakisema walikosea uteuzi wa mgombea.
“Kwa mfano pale kwangu huyo ambaye wanasema alikuwa na nguvu ni siasa tu za kwenye vyombo vya habari, lakini hakuna chochote ambacho kingemfanya ashinde 2010,” alisema Msigwa akimaanisha mgombea aliyeenguliwa kwenye vikao vya juu vya CCM, Frederick Mwakalebela.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2010, Mchungaji Msigwa alipata kura 17,740 na kumbwaga mpinzani wake kutoka CCM, Monica Mbega ambaye alipata kura 16,914. Mbega alishindwa na Mwakalebela kwenye kura za maoni, lakini alipitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Pamoja na kushinda kwa tofauti ndogo ya kura, Mchungaji Msigwa anasema ana uhakika wa kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa amebadilisha fikra za wananchi wake kwa kuwafundisha jinsi ya kudai haki zao.
“Kitu ambacho kitanibakiza ni jinsi nilivyowabadilisha mtazamo wananchi wangu na hata nikiondoka leo, hilo ndilo jambo ninalojivunia kwamba wanajitambua. Nimekuwa daraja kwa wananchi wangu kuelewa jinsi ya kujitatulia matatizo yao,” alisema Msigwa na kuongeza:
“Kuwapa msaada ni kitu kimoja lakini wao kujisaidia wenyewe ni jambo la muhimu zaidi.”
Hapa Msigwa alikuwa akizungumza kwa upole na umakini kwamba wabunge wa zamani walizoea kuwapa wananchi misaada ambayo alisema haiwezi kuwasaidia. Hata hivyo, Msigwa anasikitika kuwa awali, alitarajia bungeni angekutana na watu ambao wanaweza kujibu hoja anazozitoa, lakini akakuta hali tofauti na alivyotarajia. “Yaani kwa hilo kweli linaniumiza, watu hawajibu hoja kabisa, wanaleta siasa siasa tu. Zile suti wengine hamna kitu kabisa,” alisema kwa sauti ya chini huku akitingisha kichwa kuashiria kusikitika.

Katiba Mpya na Ukawa kususia Bunge
Kuhusu uamuzi wa vyama vya upinzani vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, Msigwa alisema kitendo hicho kimefanikisha kutimiza azma yao kwa kuwa wananchi wameweza kuelewa kwa nini walifanya hivyo.
“Tumesababisha mjadala mkubwa na wananchi wamejifunza mengi ambayo walikuwa hawaelewi. Kitu tulichofanya ni cha kijasiri japokuwa kuna watu wameumizwa na uamuzi huo, lakini ujumbe umefika,” alisema.
Alisema kitendo cha polisi kuzuia maandamano ya Ukawa katika maeneo mbalimbali nchini, kinaonyesha kuwa CCM ilihofia matokeo ya maandamano yao katika mjadala mzima wa Katiba Mpya.
Alisema Ukawa utafanya kazi kubwa zaidi kwenye kura ya maoni kuhakikisha wananchi hawapigi kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
“Tutakapofika kwenye kura ya maoni tutawaonyesha kuwa walivyocheza dansi pale bungeni, waliwakosea wananchi. Watashindwa kwenye kura hiyo kwa kuwa walicheza kufurahia kuwa na wabunge wasio na elimu.”
Msigwa alisema nchi iko tayari kubadilika, lakini CCM haitaki kukubali mabadiliko kwa kuwa inatumia mbinu za zamani.

Ujangili
Kuhusu ujangili, Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, alisema ni tatizo nchini kwa kuwa wanaofanya biashara hiyo ni watu wakubwa.
Alisema watu hao wengine ameshawataja, lakini bado tatizo linaendelea hivyo ni lazima itumike njia nyingine ya kuweza kupambana na watu hao.
“Wengine nilishawahi kuwataja na wamenifikisha mbali, nitaendelea na mapambano kuhakikisha ujangili unatokomea,” alisema.
Msigwa alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa zilizokuwa zikienea kuwa amekuwa na ugomvi na mawaziri wawili waliopita wa Wizara ya Maliasili na Utalii akisema: “Sijawahi kuwa na ugomvi na Ezekiel Maige wala Khamis Kagasheki kwa kuwa wajibu wangu kama kiongozi ni kusimamia yale yaliyo sahihi.” Alisema tatizo mojawapo la mawaziri hao ni kufanya mambo kwa siri, hivyo kuzua maswali mengi kwa watu.
“(Waziri wa sasa) Lazaro Nyalandu yeye tunashirikiana katika kila jambo ambalo linahitaji waziri kivuli, hiyo inatoa nafasi kuelewa mambo mengi kwa kuwa ninauona upande wa pili, lakini akifanya makosa ninambana,” alisema Msigwa.
“Hivi sasa kuna suala la uvunaji magogo ambalo ni tatizo kubwa, hivyo ni lazima Nyalandu alishughulikie kwani huo ndiyo uwajibikaji.”

Uchungaji na siasa
Msigwa, ambaye alisomea uchungaji huko Afrika Kusini, alisema kabla ya kuwa mchungaji alikuwa mfanyabiashara wa mitumba na wakati akitekeleza majukumu hayo, alijisikia kumtumikia Mungu kwa njia ya mahubiri.
Kutokana na wito huo, alianza kutangaza Injili katika shule mbalimbali mkoani Iringa huku akiendelea na biashara zake. “Baadaye nilipata nafasi ya kwenda kusomea uchungaji Afrika Kusini na niliporudi nikawa natoa neno la Mungu na baadaye nikaingia kwenye siasa,” alisema Msigwa.
Alisema pamoja na kwamba yuko kwenye siasa, bado anaendelea na shughuli zake za kichungaji kwa kuwa amejipangia muda wa kufanya hivyo.
“Napata nafasi ya kutoa elimu kanisani, wakati mwingine ninaalikwa sehemu mbalimbali kutoa neno na ninaendelea na siasa zangu,” alisema Msigwa.


No comments:

Post a Comment