Thursday, September 18, 2014

Safu mpya uongozi Chadema yapatikana

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata safu mpya ya viongozi wake kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

Safu hiyo imekalilishwa na uchaguzi mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam zaidi ya wiki moja iliyopita, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibroad Slaa, kwa mara nyingine akiteuliwa kuendelea kushika nafasi yake hiyo ya juu ya utendaji.

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara ilichukuliwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi.

Kabla ya uchaguzi huo, nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara ilikuwa wazi kufuatia kusimamishwa uongozi kwa aliyekuwa anaishikilia, Zitto Kabwe, Novemba mwaka jana.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, nafasi hiyo ilichukuliwa na Salumu Mwalimu, Mwandishi wa habari na mtangazaji wa kituo cha Channel Ten.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, Baraza Kuu kabla ya kupitisha uteuzi huo wa katibu na manaibu wake kama ulivyopendekezwa na Mwenyekiti wa chama hicho kwa mujibu wa katiba, lilipiga kura kuwachagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu itakayoongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano.

Uchaguzi huo uliokamilika juzi saa 5:35 usiku, ulikuwa na mchuano mkali huku baadhi ya makada mashuhuri wakiangushwa.Wanachama saba walikuwa wanawania nafasi ya kundi A bara, lakini waliochaguliwa ni watatu ambao ni Mabere Marando aliyepata kura 164, Prof. Mwesiga Baregu kura 127 na Dk. Yared Fubusa kura 127.

Walioangushwa ni Deogratias Munisi (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Bavicha), Fred Mpendazoe, Hebron Mwakagenda na Edson Wakili Mbogoro.

Katika kundi B wanawake bara waliowania ni watano, lakini waliochaguliwa ni Catherine Vermand aliyepata kura 97 na Suzan Kiwanga aliyepata kura 93, huku Angela Lima, Chiku Abwao na Cecilia Pareso wakiangushwa. Abwao na Pareso ni wabunge wa Viti Maalum.

Kwa upande wa kundi C, wanaume upande wa Zanzibar, waliowania ni wawili na aliyechaguliwa ni Salum Mwalimu kwa kura 112 aliyemwangusha Nassor Salim.

Hata hivyo, nafasi ya Salum Mwalimu ilibaki wazi baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Kundi D, wanawake kutoka Zanzibar waliowania ni wawili, lakini aliyeshinda ni Zainab Mussa Bakari kwa kura 111, huku Dhifa Mohamed Bakari akiangushwa.

Katika kundi la watu wenye ulemavu ambalo lilikuwa na mgombea mmoja, aliyeshinda ni Elly Marco Macha kwa kupata kura 154.

Wakati huo huo, Makene alisema Kamati Kuu ya Chadema ilikutana jana kujadili ajenda tatu moja ikiwa ni yale yaliyotokana na Baraza Kuu, mwelekeo wa mchakato wa Katiba na uchaguzi wa serikali za mitaa.

No comments:

Post a Comment