Monday, September 22, 2014

Mnyika amtaka Rais Kikwete alivunje Bunge Maalumu

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kulivunja Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.

Aidha, amemtaka Rais kuitisha Bunge la kawaida ili uchaguzi mkuu mwakani uwe huru na haki.

Mnyika alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana wa vyama rafiki wa Chadema lengo likiwa ni kuwaandaa kwenye masuala ya uongozi. Mafunzo hayo ambayo ni mwendelezo wa yale ambayo hutolewa na Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA), safari hii yamehusisha vijana kutoka Kenya, Uganda na Tanzania.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema vijana wa Tanzania na Uganda wanatakiwa kujifunza kutoka Kenya ambao waliingia kwenye machafuko baada ya kufanya Uchaguzi Mkuu kabla ya kupata Katiba Mpya.

Alisema matokeo yake viongozi wake wa juu walifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, (ICC). Alisema Kikwete anatakiwa atoke kwenye siasa na kuvaa nafasi ya kiongozi ili kunusuru hayo yaliyotokea Kenya yasijitokeze hapa.

Kuhusu vijana wa nchi za Afrika Mashariki, Mnyika alitaja changamoto inayowakabili kuwa ni ajira ambayo aliwataka waliobahatika kupata mafunzo hayo, watoke na mkakati wa kufanya kampeni ya kupunguza tatizo hilo.

Aliigusia nchi ya Libya na nyingine duniani ambazo zinapigana vita huku akisema moja ya sababu ya machafuko ni pamoja na ukosefu wa ajira.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Patrobass Katambi, alisema wanataka katiba inayokubaliwa na Watanzania wote ambayo itakuwa na tija kwao.

Kuhusu maandamano ya Chadema yanayoendelea nchini huku jeshi la polisi likiyazuia kwa kuwakamata, mwenyekiti huyo alisema matendo ya chama tawala ya kutumia dola vibaya ndiyo yanayosababisha vurugu na kutokea vita.

No comments:

Post a Comment