Tuesday, September 30, 2014

Chadema wafunika Mwanza, polisi watawanywa kwa mabomu

Baada ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kuzuia maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katikati ya wiki iliyopita, umati mkubwa wa wakazi jijini hapa jana walifurika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani kuwasikiliza viongozi wao wa kitaifa.

Viongozi hao ni Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.Mkutano huo uliohutubiwa na viongozi hao, pia ulihudhuriwa na viongozi wa mkoa wa Mwanza wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) ambavyo pamoja na Chadema  wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo, walikuwa wamevaa sare za vyama vyao vinavyounda Ukawa na  muda wote walionekana kuwashangilia viongozi wao walipopanda jukwaani.

Mnyika alisema baada ya serikali kuzuia maandamano yao nchi nzima kupinga Bunge Maalum la Katiba, sasa wametangaza mbinu mpya ya kuandamana kwa njia ya kutuma ujumbe mfupI wa simu (sms) na kwamba watakapoandamana na kuzuiliwa waandamanaji watakuwa wanatuma sms kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo, Andrew Chenge, ili kufikisha ujumbe wao.

Kwa upande wake, Mwalimu alisema vyama vitatu vinavyounda Ukawa ni lazima wawe wamoja kuhakikisha upatikanaji wa katiba mpya aliyoiita ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukwame na kuwataka wanachama kujitokeza pale yanapokuwapo maandamano kwa ajili ya kufikisha ujumbe.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Ilemela, Wanzagi Warioba, alisema ni wakati sasa wa vyama hivyo vinavyounda Ukawa kuunganisha nguvu ya pamoja kuwaondoa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na kuwatumia polisi kuwadhibiti wapinzani.

“Ni muda wa kuungana ili kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji, kuwang'oa kabisa hawa CCM ambao wanaamini nchi hii ni mali yao pekee yao,” alisema Warioba.

Naye Kamishana wa NCCR-Mageuzi mkoa wa Mwanza, Amran Ramadhani, alisema wakati wa mapambano na wadhalimu wa nchi hii kuwaondoa viongozi wa CCM umewadia, hivyo wananchi wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja na Ukawa kuwaondoa.

“Pale Chadema watakaposimamisha mgombea, lazima vyama vingine tumpe nguvu mgombea huyo, na CUF nao vile vile na NCCR-Mageuzi hivyo hivyo, hakuna kuwaachia nafasi hawa CCM kuchukua uongozi katika ngazi yoyote,” alisema Ramadhani.

Katibu Mwenezi wa CUF mkoa wa Mwanza, Hamza Shido, alisema muda wa mapambano dhidi ya polisi na CCM umewadia kutokana na watu hao kuwasumbua sana wananchi wasio na hatia yoyote.

" Tunaandamana bila silaha, lakini tunavurumishiwa mabomu na kukamatwa ovyo...sasa ni wakati wa kupigania haki zetu kwa namna yoyote ile,” alisema Shido.

Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje, alisema muda wa kuwaondoa viongozi wa CCM katika uongozi ni sasa mara baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.

“Tumenyanyaswa sana na polisi wa CCM, sasa tumefikia mwisho kwani wanaelewa ni jinsi gani ambavyo wataondolewa madarakani na wananchi... tunatengenez barabara, lakini wao wanasema ni sera ya CCM, sasa mbona wabunge wao walikuwapo hawakuufanya hivyo?” alihoji Wenje.

Hata hivyo baada ya mkutano huo kumalizika askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Mwanza, walitumia mabo,u kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiwasindikiza viongozi wao wakiwa katika makundi.

No comments:

Post a Comment