Saturday, July 12, 2014

SAMUEL SITTA ANATAFUTA THELUTHI MBILI AU MWAFAKA?

Kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samuel Sitta amenukuliwa leo akisema kuwa ameunda Kamati ya Mashauriano ili kuondoa alichokiita ni mpasuko kati ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na Umoja ya Katiba ya Wananchi (UKAWA) na wajumbe wengine.

Kwa mujibu wa habari hizo Sitta amenukuliwa akisema kuwa kamati yake yenye wajumbe 27 itakutana Julai 24, mwaka huu ambapo amesema kuwa watajadili mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za Rasimu ya Katiba Mpya, ili ‘eti’ kujua yapi muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya Bunge Maalum la Katiba kuanza vikao vyake hapo Agosti 5, mwaka huu.

Taarifa hiyo ya Sitta akiwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba imedhihirisha masuala kadhaa, kama ifuatavyo;

1. Hajui anachokitafuta

Wakati katika hali ya juu inaweza kudhaniwa kuwa Sitta anatafuta suluhu yenye kuleta maridhiano na hatimaye mwafaka wa kitaifa kwenye suala la Katiba Mpya, taarifa hiyo ikisomwa kwa makini na kina, inaonesha namna ambavyo ‘harakati’ zake hizo ni mwendelezo wa hila za watawala kusaka Katiba Mpya kwa kura, badala ya maridhiano yanayosimamia maoni, maslahi na matakwa ya wananchi.

Moja ya vyombo vya habari vilivyoripoti taarifa hiyo ya Sitta, kimeandika;

“Pamoja na mambo mengine, Sitta alisema upo uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini wakasusa tena kadiri mjadala utavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya maamuzi.”

Kauli hiyo inadhihirisha kuwa Sitta kama Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, tena mwanasheria kwa taaluma na sasa mwanasiasa, hajielekezi katika kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inakidhi moja ya vigezo muhimu sana ambavyo ni kuwa na uhalali wa kisiasa unaotokana na maridhiano au mwafaka wa kitaifa.

Na hii ndiyo sehemu kubwa inapolalia hila ya walioko madarakani, wakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupanga kutumia wingi wa kura kuamua suala nyeti la Katiba Mpya kwa sababu tu wanapigania kuhakikisha matakwa ya CCM yanawekwa mbele kutokana na maelekezo ya vikao vya chama hicho, vilivyotoa nyaraka zikitaka ‘mambo’ ya CCM ndiyo yawe Katiba Mpya.

Ni mwendelezo wa hila za walioko madarakani kutaka kutumia hila za kura badala ya maridhiano, kupitisha matakwa na misimamo ya viongozi wa CCM huku maoni, maslahi na matakwa ya wananchi kama walivyoyawasilisha mbele ya Tume ya Jaji Warioba yakiwekwa kando, kubezwa na kudharauliwa.

2. Kuendeleza lugha ya dharau, kubeza

Aidha, wakati kupitia taarifa hiyo, Sitta anataka kujipambanua kuwa msaka suluhu na maridhiano, lakini ameshindwa kuficha uhalisia wake, ambapo ameendeleza tabia ile ile ya Wajumbe wa BMK wanaotokana na CCM (au wanaounda Kundi la Tanzania Kwanza), kutumia lugha ya kebehi na dharau kwenye jambo nyeti linalohitaji masikilizano, ikiwemo matumizi ya maneno na lugha.

Hilo linadhihirika pale aliponukuliwa akisema “kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti, atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua nia yake ni tofauti na Katiba Mpya.”

Kwa mtu yeyote makini, hawezi kuamini kuwa maneno hayo yanaweza kutumiwa na mtu anayetaka kuonekana anasaka suluhu kwenye jambo nyeti kama Katiba!

Lakini pia maneno hayo yanaibua shauku zaidi ya kujua; kwa nini Sitta tayari anaonekana kuwa ‘defensive’ kwamba kuna viongozi watadharau huo wito wake au uteuzi wake?

Je Sitta amefanya uteuzi huo kama nani kuweza kupata watu 27nchi nzima?

Je Sitta ameanza kushtukia uhalali wa uteuzi wake huo ambao haujulikani kaufanya lini, wapi, katika mazingira gani, akimhusisha nani?

Je anajishtukia kuwa ameteua watu ambao hawatakubalika?

Je hao viongozi wa dini ambao amewateua ni wale wale ambao tayari tumewasikia ndani ya BMK wakisahau wajibu wao katika jamii, (maaskofu, wachungaji na mashehe) kisha wakatoa misimamo yao hadharani kuungana na CCM dhidi ya wananchi?

Ni watu gani hao hasa ambao Sitta amewateua kisirisiri akitaka wasimame kuwa wasuluhisi chini ya mwamvuli wake?

Swali jingine muhimu, Je kwa kitendo cha Sitta na wenzake kuendelea kuonesha msimamo wao kinyume cha maoni ya wananchi wakati huo huo wanawateua viongozi wa dini kujadili suala hilo hilo kwa mlengo wanaoutaka wao (akina Sitta) Je sasa wameamua hata kuwachonganisha viongozi wa dini na waumini wao? Kwa sababu waumini ni hao hao Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ambayo CCM wameyabeza na kuyadharau hadharani!

3. Tayari anao upande wake

Aidha, kitendo cha Sitta kupitia taarifa hiyo kujaribu kuonesha au kulazimisha taswira kuwa tatizo la mkwamo huu wa Katiba Mpya ni UKAWA, kuamua kutoliangalia jambo hili katika ‘picha pana’ na kulichukulia kwa uzito wake.

Ni matokeo ya kutopenda kuutafuta, kuuona na kuukiri ukweli hata kama unauma.

Watanzania wote ambao wanafuatilia mchakato huu wa Katiba Mpya kama moja ya fursa adhimu za kujiumba kama taifa, watashangaa kuona Mwenyekiti wa Katiba hajui kuwa CCM, tena kupitia maamuzi ya vikao vya chama hicho na kauli za Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ndiyo zimekwamisha mchakato huu nyeti.

Kwamba kupitia vikao vyao vinavyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, chama hicho kilitoa maelekezo kwa nyaraka za siri kikitaka wajumbe wanaotokana nacho wasimamie misimamo ya chama. Nao wakafanya hivyo kwa dharau, kubeza na kutukana maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyowasilishwa na Jaji Warioba.

Wananchi wanajua kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutumia nafasi yake ya ukuu wa nchi wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba Mpya kuliongoza taifa zima kujadili Rasimu ya Pili, kwa kuzingatia maoni ya wananchi, badala yake akatumia wadhifa wa uenyekiti wa chama kuweka misimamo ya kichama inayotokana na vikao vya chama alivyovisimamia, ni moja ya vigingi vilivyokwamisha na kuharibu mchakato huu.

Tayari, kutokana na taarifa za ziada na kina zilizopo, tunajua kauli hizo au hali hiyo ya kuwa na upande anayoionesha Sitta si jambo la bahati mbaya.

CCM kupitia taarifa yao maalum kuhusu mwenendo wa BMK, wanakiri kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Marekebisho ya Katiba Sura ya 83, ili Bunge Maalum liweze kupitisha vifungu vya Katiba ni lazima zipatikane theluthi mbili za kura kwa pande zote za Muungano, lakini kutokana na msimamo wa UKAWA kusimamia misingi ya uandishi wa katiba, maoni, maslahi na matakwa ya wananchi, CCM wameshindwa kutimiza malengo yao.

Sasa anachofanya Sitta kwa ghiliba na hadaa ya kutafuta suluhu ni kuanza kufanya maandalizi ya namna ya kuharibu mchakato kwa ‘kuchezea’ kifungu hicho cha sheria.

4. Kuendelea kudharau msingi wa Rasimu ya Katiba

Mwenyekiti wa BMK Sitta pia kupitia taarifa hiyo ameendeleza kauli zile zile ambazo zimekuwa zikitolewa na wajumbe wa bunge hilo wanaotokana na CCM, ambazo hasa ndizo zilikuwa moja ya sababu kubwa kwa UKAWA kutoka nje kususia vikao vile.

Amenukuliwa akisema “yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo…ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee.”

Huu ni mwendelezo wa dharau dhidi ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Sitta akiwa Mwenyekiti wa BMK na mwanasheria anajua wazi kuwa msingi wa rasimu hiyo ni uwepo wa Muundo wa Shirikisho la Serikali, sasa msuluhishi (kama mjenzi) anawezaje kubeza umuhimu wa msingi lakini akang’ang’ania kuendelea kujenga ukuta, kuweka madirisha, milango, paa na vingine vyote vinavyokamilisha ujenzi wa namna hiyo? Mambo hayo yako kwenye hadithi. Labda kama Samuel Sitta anataka kugeuza jambo hili nyeti kuwa ni sawa na Hadithi za Abunuwas!

5. Maneno yale yale; yeye, Mangula na vijana wao

Kama ambavyo kwa nyakati tofauti viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa viroja (badala ya hoja) na propaganda mbalimbali dhidi ya UKAWA wakijaribu kuhamisha mjadala kwa kuibua tuhuma zisizokuwa na msingi, Sitta naye ametumia mtindo huo huo hali ambayo inaonesha kuwa mambo haya yanapangwa na CCM kwa lengo lile lile; kuhakikisha Katiba Mpya haipatikani.

Amenukuliwa akisema “Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya siri.

““kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti, atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua nia yake ni tofauti na Katiba Mpya.”

Mpango huo wa kuzusha tuhuma hizi mara zile, zikitumia maneno kama hayo aliyotumia Samuel Sitta umekuwa ukitumika na viongozi wa CCM mara kadhaa sasa. Makamu Mwenyekiti Phillip Mangula (ambaye baadae alikanusha) na vijana wao kama Nape Nnauye na wengine wamesikika mara kadhaa wakitoa tuhuma za uongo dhidi ya UKAWA, kuhusu hongo au kutumiwa kuvuruga mchakato.

Propaganda na hila hizi hazitasaidia. Wananchi wanajua aliyekwamisha mchakato huu. Mtu anayetaka kuwa msuluhisi anapoingia akiwa na ‘sentiments’ kama hizo ambazo zinaimbwa kila siku majukwaani na viongozi wa CCM kwa lengo la kuhadaa na kughilibu umma, anakuwa tayari amejipungizia uhalali wa yeye kutiliwa maanani na kutoa mwanya wa umakini wake kuhojiwa.

Tumkumbushe Sitta na wenzake waliozoea kuendesha mambo kwa hila na propaganda, msimamo wa UKAWA ambao haujayumba na mara kadhaa sasa umesisitizwa na viongozi waandamizi, akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, James Mbatia, ni kwamba; Rasimu ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi iheshimiwe.

Bunge Maalum la Katiba lina kazi ya kujadili na kupitisha rasimu hiyo, mjadala unapaswa kuongozwa kwa kuzingatia hilo bila kusahau kuwa kiini au msingi wa rasimu hiyo ni kuwepo kwa Muundo wa Shirikisho la Serikali tatu. Hayo ndiyo maoni ya wananchi ambayo UKAWA umeamua kuyasimamia.

Imetolewa Jumatano, Julai 9, 2014 na;

Tumaini Makene



Mkuu wa Idara ya Habari-CHADEMA

No comments:

Post a Comment