Saturday, July 19, 2014

MNYIKA AIWEKA MTEGONI WIZARA YA MAJI MBELE YA WANANCHI

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika ameiweka mtegoni Wizara ya Maji, akiitaka iweke wazi kwa umma, ratiba ya ziara ya kikazi ya wizara hiyo kujionea tatizo la maji katika jimbo hilo na maeneo mengine jijini Dar es Salaam ili wananci waweze kuhudhuria na kushiriki kikamilifu.

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge, ikisainiwa na Katibu Msaidizi, Aziz Himbuka, Wizara ya Maji pia imetakiwa kuweka wazi ripoti ya matokeo ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi mmoja kuanzia Mwezi Mei kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa mengine ya kibinadamu.

Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo imesema kuwa ratiba hiyo inapaswa kujulikana kwa umma kwa sababu mbali ya kuhusisha kutembelea mitambo ya kusafirisha, kusukuma na kusambaza maji, itahusisha pia mikutano ya wananchi, ambayo imeelezwa kuwa ni muhimu ikajulikana ratiba yake mapema ili wananchi waweze kushiriki.

Katika taarifa hiyo Ofisi ya Myika imesema kuwa kufuatia hatua ambazo mbunge huyo alichukua katika mkutano wa 15 wa Bunge uliomalizika karibuni juu ya matatizo ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na DAWASA na DAWASCO hususan kutoka vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, Wizara ya Maji ilirekebisha baadhi ya kasoro na kuahidi kuongeza kasi zaidi ya kazi ya kuongeza mgawo wa maji.

Taarifa ya Katibu wa Mnyika iliongeza kusema kuwa pamoja na hatua hiyo kusaidia ongezeko la upatikanaji wa wa maji katika baadhi ya maeneo, imesema kuwa bado yapo maeneo yanayohitaji hatua za ziada.

“Hivyo, Wizara ya Maji inapaswa kutoa taarifa kwa umma juu ya ratiba ya ziara ya kikazi ya Waziri au Naibu Waziri wa Maji katika Jimbo la Ubungo na maeneo mengine ya Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani kuanzia wiki hii kuendelea kusimamia kasoro zilizopo zirekebishwe.

“Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inakumbusha umma kwamba Naibu Waziri wa Maji Amos Makala aliahidi bungeni wakati akimjibu mbunge kwamba ziara ya kikazi itaanza tarehe 14 Julai 2014.

“Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inatambua kwamba Wizara iliwasilisha mapendekezo ya awali ya ratiba ya ziara kwa mbunge akiwa bungeni Dodoma na mbunge kupendekeza marekebisho ya ratiba kuongeza maeneo ambayo ni muhimu kufikiwa kuongeza upatikanaji wa maji. Hata hivyo, mpaka leo tarehe 13 Julai 2014 Ofisi haijapokea ratiba ya mwisho toka Wizara ya Maji juu ya ziara hiyo,” imesem tarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mbunge wa Ubungo.

Kuhusu ripoti ya uchunguzi uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi mmoja (Mei), kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya Mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa mengine ya kibinadamu, Ofisi ya Mnyika imesema kuwa wizara inawajibika kutimiza ahadi iliyotolewa bungeni wakati wa vikao vya bajeti hivi karibuni.

“Mwezi Juni 2014 Mbunge wa Ubungo, alitaka taarifa hiyo iwasilishwe na Naibu Waziri wa Maji Amos Makala alijibu kwamba tayari Kamati hiyo imeshamaliza kazi yake na kukabidhi ripoti hiyo kwa Wizara. Naibu Waziri aliahidi kwamba ripoti hiyo ingetolewa hivyo ni muhimu kupitia ziara hiyo ya kikazi ripoti hiyo ikatolewa kwa Mbunge na kwa wananchi,” imesema taarifa hiyo ya Himbuka.

Akiweka msisitizo kuhusu ripoti hiyo kuwekwa wazi, Himbuka alirejea kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni hivi karibuni na Waziri wa Maji alipojibu mwongozo ulioombwa na Mnyika, ambapo Prof. Jumanne Maghembe alikiri kwamba kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014 na tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango na kufikia kati ya lita milioni 8.2 na lita milioni 57.4 ikilinganishwa na lita milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo.

“Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa Ruvu Juu kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60), kukatika kwa Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu wa upatikanaji wa vipuri halisi.
“Hata hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya madai ya kuwepo kwa udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo vya maji na mitandao ya mabomba ya maji,” alisema Himbuka kupitia taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment