Saturday, April 19, 2014

UKAWA wapigwa marufuku mkutano Zanzibar

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa ambao ulipanga kuunguruma leo katika mkutano wa hadhara Viwanja vya demokrasia Kibandamaiti visiwani hapa, umenyimwa kibali kwa madai ya kuwapo kwa tishio la ugaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadamu Khamis Mkadamu, alisema awali Ukawa uliruhusiwa kufanya mkutano huo lakini kutokana na tishio hilo, polisi imekataza .

“Sababu ya kukataza mkutano huo usifanyike kuna kikundi cha ugaidi kimetishia hali ya usalama na ndiyo maana wamezuiwa,” alisema na kuongeza kuwa wamezuiwa mpaka hapo watakapotoa kibali kingine.

UKAWA WATOA TAMKO
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye pia ni mwanachama wa Umoja huo, amesema sababu wanazotoa polisi ni zile walizokuwa wanatoa miaka 20 iliyopita wakati Tanzania inaingia kwenye mfumo wa vyama vyama vingi.

Alisema Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria ya nchi haliruhusiwi kufanyakazi kwa niaba ya chama cha siasa kwa sababu linalipwa mshahara kutokana na kodi za wananchi.

“Kama kuna tishio la ugaidi ni kazi yao kulinda, kama wameshindwa kukamata magaidi pale Arusha, wasisingizie mkutano wa Zanzibar,” alisema.

Alisema sababu wanazotoa polisi kuzuia mkutano huo ni kama walizozitoa wakati vyama vya upinzani vilipotaka kufanya mkutano wake Jangwani, lakini mkutano ulifanyika na hakuna lolote lililotokea.

“Tumeshaingia gharama kubwa ya kuandaa mkutano huo hatuwezi kukubali,” alisema .

Alipoulizwa kama Ukawa itaendelea na mkutano wao kama walivyopanga, Mbatia alisema kwa kuwa viongozi wote wapo Dar es Salaam, suala hilo watalizungumzia leo watakapokuwa eneo la tukio. 

Awali akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi wa mawasialiano ya umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Salim Bimani, alisema umoja huo umeomba kibali na kuruhusiwa na jeshi la polisi kwa masharti maalum.

Alisema masharti waliyopewa ni kutotoa maneneo ya kashfa, kutofanya uchochezi na kulinda amani na utulivu wa nchi.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuzungumzia mambo mbalimbali ikiwemo kutoa ufafanuzi kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na mchakato unaoendelea katika Bunge la Katiba mjini Dodoma.

Mkutano huo ulikuwa uhudhuriwe na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa vya upinzani ikiwemo CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ni miongoni mwa viongozi waliokuwa wahutubie mkutano huo.

Umoja huo juzi ulisusia kikao cha Bunge Maalum la Katiba kwa kile walichodai kuwa umechoshwa na matusi, vijembe na mipasho kutoka kwa wajumbe wanaotoka Chama cha Mapinduzi.

Umoja huo ulidai kuwa hauwezi kurudi kwenye vikao vya bunge hilo hadi muafaka utakapopatikana kutokana na hali hiyo.

Aidha, Umoja huo ulisema utafanya mikutano ya nchi nzima kwa ajili ya kuwashtaki wananchi kile kinachoendelea bungeni. Pia Umoja huo unakusudia kueleza umma msimamo wao dhidi ya Bunge hilo walilodai limepuuza kile Watanzania walichopendekeza kwenye Tume ya Jaji Warioba.

No comments:

Post a Comment