Sunday, April 6, 2014

HALI ILIVYOKUWA NA MATOKEO YA AWALI CHALINZE

Uchaguzi wa mdogo wa Jimbo la Chalinze umefanyika huku ukigubikwa na kasoro kadhaa, ikiwa ni pamoja na watu wachache kujitokeza vituoni kupiga kura, wapiga kura kulalamika ‘kupokwa’ vitambulisho vyao, vituo kuwa majumbani kwa watu, huku pia kukiwa na hofu ya vurugu.

Kasoro hizo zilijidhihirisha jana wakati wapiga kura shughuli ya upigaji kura ilipokuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ambapo wananchi wa Chalinze walikuwa wakipiga kura mbunge wao, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki mapema mwaka huu.

Gazeti hili liliweza kuzunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura ambapo lilishuhudia idadi ya watu wachache wakiwa wamejitokeza kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Katika kituo cha kupigia kura, Ofisi ya Maji Changa namba 2, hadi muda wa kufunga vituo ukiwa umebakia nusu saa, walikuwa wamejitokeza wapiga kura 75 kati ya 328 walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Kituo hicho, kilikuwa miongoni mwa vituo kadhaa vilivyokuwa majumbani mwa watu, kikiwa katika nyumba ya Mzee Issa Mbogo, kinyume cha sheria ya uchaguzi.

Katika kituo cha Tukamisasa hadi muda wa kufunga vituo ukiwa unakaribia mwisho, yalikuwa yametukika madaftari mawili pekee, kati ya madaftari sita ambayo yalipaswa kuwa kituoni hapo, ambapo kila daftari linajumuisha wapiga kura 50.

Mbali ya vituo kama hivyo ambavyo viko maeneo ya vijijini, hata vituo vilivyokuwa kata za mjini kama Builingu, pia hazikuwa na wapiga kura wengi.

Mathalani Kituo cha Ofisi ya Mtendaji Namba 2; waliopiga kura walikuwa 64 kati ya wapiga kura 383, Namba 3; waliopiga kura ni 62 kati ya 383.

Kata nyingine ya Pera ambayo pia iko maeneo ya mjini, Kituo cha Shule ya Msingi Namba 1; waliopiga kura ni 88, kati ya walioandikishwa 443, Kituo cha Pera Shule ya Msingi Namba 2; waliopiga kura ni 100 kati ya wapiga kura 443.

Kituo cha Chamulungu Namba 1; waliopiga kura 100 kati ya 336, huku Chamulungu II wakipiga kura 88 kati ya 325.

Wapiga kura kupokwa vitambulisho

Baadhi ya wapiga kura katika kata ya Ubena, walitoa malalamiko yao wakimtuhumu Katibu wa CCM Tawi la Lulenge kwamba alifika majumbani mwao wakati wanaume hawapo na kuchukua vitambulisho vya kupigia kura akisema kuwa anakwenda kuandikisha namba zao.

Akizungumza kwa uchungu mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la alisema kuwa kitendo hicho hicho si sahihi na akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki.

“Hapa unavyoniona nimeshindwa kupiga kura hadi sasa…jina langu na namba yangu vipo kwenye daftari kwenye kituo kile pale, lakini sina kitambulisho. Juzi natafuta kitambulisho change, mke wangu ananiambia alikuja Rajab Said ambaye ni Katibu wa Tawi la CCM Lulenge, eti alikwenda kuandikisha namba zetu.

“Hadi muda huu ninaokuambia, hajarudisha vitambulisho kwa sababu siko peke yangu, kuna wengine kama 9 hivi ninawafahamu nao pia vimechukuliwa,” alisema Simon Pojoro.

Kwa upande wake Said akijibu tuhuma hizo, Said alisema kuwa madai hayo si kweli nay eye hajui suala hilo wala hakuhusika kwa namna yoyote kwa wapiga kura kukosa haki yao ya kuchagua mbunge wao, akisema huo ni uzushi.

Tuhuma za gari ya CCM ‘kumwinda’ mgombea wa CHADEMA

Wakati huo huo, akizungumzia mwenendo wa uchaguzi huo, mgombea ubunge wa CHADEMA, Mathayo Torongey alisema kuwa gari aina ya Land Cruiser ‘hard top’, T 630 BFJ, inayomilikiwa na CCM, ilikuwa ikimfuatilia kila mahali alikokwenda wakati akipita maeneo mbalimbali kukagua vituo, kama sheria inavyomruhusu.

“Tena bahati nzuri nimefika hapa kupita kwenye hiki kituo nimeikuta hii gari, hii ndiyo imekuwa ikinifuatilia tangu asubuhi. Wamekuja pale Mdaula akashuka kijana mmoja...yule pale…akiwa na sime na nondo, tulipomshtukia akarudi ndani ya gari akabadili nguo akavua tisheti ya bluu aliyokuwa nayo akavaa koti hilo la kijeshi kama mnavyomuona hapo,” alisema Torongey huku akionesha gari na huyo mtu.

“Tunashukuru kuwa kulikuwa na polisi pale, tuliwapatia taarifa naona wamechukua hatua, tumelikuta gari hili likiwa liko hapa na hawa askari, lakini nashangaa hawajapelekwa kituoni na unawasikia wanavyozungumza kwa jeuri mbele ya polisi,” aliongeza.

Mbele ya waandishi wa habari, gari ile iliyokuwa na watu wengi ndani, huku kuionekana silaha mbalimbali na bendera ya CCM, iliruhusiwa kuondoka maeneo hayo, ikiamriwa ielekee kituoni (bila kusindikizwa na polisi), ambapo kiongozi mmoja, ambaye ni katibu wa chama hicho wilaya moja ya Iringa, akijigamba kwa kusema ‘tutakwenda kituoni baada ya kumaliza kazi zetu.”

Matokeo ya awali

Kata ya Pera; Malivundo Ofisi ya Mtendaji; CCM 77, CHADEMA 2, CUF , AFP 1, NRA 1.
Kimbugi; CCM 11, CHADEMA 1, CUF 0, AFP 0, NRA 0
Magange Ofisi ya Kitongoji; CCM 101, CHADEMA 1, NRA 0, AFP 0
Pingo Shule ya Msingi Namba 1; CCM 31, CHADEMA 1, CUF 1, NRA 0, AFP 0  
Pingo Ofisi ya Kitongoji Namba 2; CCM 61, CHADEMA 4, CUF 2, AFP 1, NRA 0

Pingo Namba 1; CCM 66, CHADEMA 0, NRA 0, AFP 0

No comments:

Post a Comment