Saturday, August 9, 2014

WAWILI WATOA USHAHIDI WA NJAMA HARAMU DHIDI YA VIONGOZI WA JUU WA CHADEMA


Picha za leo wakati Sebastian Peter Mzuka na Zacharia Martine Mfuko, walipoweka wazi mkakati mzima wa kulipua chopa iliyowabeba Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Slaa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar Said Issa Mohamed, Mbunge wa Ubungo John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Mashariki Sylvester Kasulumbayi mbele ya waandishi wa habari leo. Pia waliweka hadharani mkakati unaopangwa na CCM kwa kutumia tawi lake jipya la ACT kujaribu kuua upinzani nchini hasa kwa kudhoofisha CHADEMA.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WABUNGE WA CHADEMA KUONEKANA DODOMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU WABUNGE WA CHADEMA KUONEKANA DODOMA

Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.

Chama kupitia Idara ya Habari kingependa kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;

1. Uamuzi wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi mchakato wa Katiba Mpya, ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu iliyoketi Julai 18-19 na kuazimia kwamba;

Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka ya Bunge hilo yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta, misingi mikuu (basic features) ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais kwa ajili hiyo;

Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA, kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na baada ya, ufafanuzi uliotajwa katika aya ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge Maalum, pamoja na Kanuni husika za Bunge Maalum;

Wajumbe wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum hawatashiriki katika kikao chochote cha Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum uliotajwa katika aya za 2 na 3 utakapofanyika kwa mujibu wa maazimjo ya Kamati Kuu;

Hadi wakati huu, hakuna jambo hata moja kati ya hayo lililofanyika, huku mazungumzo yaliyotarajiwa kuokoa mchakato yakiwa yamevunjika, kwa sababu CCM na Serikali yake wameamua kudharau na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba badala yake kuweka maslahi ya chama hicho kwenye katiba.

2. Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au watashiriki vikao vya bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya kujieleza kisha chama kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake kupitia vikao.

3. Tunapenda pia kuwakumbusha wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa Watanzania kuwa, mji wa Dodoma mbali ya kuwa Makao Makuu ya Nchi pia inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba ambako hakujaridhiwa na Watanzania wengi, hakujazuia shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanyika ikiwemo kutoa huduma kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wabunge. Suala hilo linakwenda sambamba na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watumishi wa Bunge Maalum la Katiba ni wale wale ambao wanatakiwa kuwahudumia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba.
Hivyo kuonekana kwa mbunge yeyote wa CHADEMA mjini Dodoma au kwenye viwanja au Ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mbunge husika amehudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kinyume na msimamo wa UKAWA.

Imetolewa leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari- CHADEMACHIKU ABWAO; NITAKUWA WA MWISHO KUISALITI CHADEMA

Kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, Dodoma Hotel, Mjumbe wa Kamati ya Chama na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao ametoa kauli nzito akisema atakuwa mtu wa mwisho kusaliti CHADEMA na siasa za mabadiliko kwa ujumla.

Abwao ambaye ni mmoja wa akina mama shupavu na imara wa CHADEMA akiwa ametumikia Watanzania kwenye siasa za mabadiliko tangu miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi, amesema hawezi kwenda kinyume na maamuzi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao umeazimia kusimamia maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.

Mbunge huyo amelazimika kuweka kumbukumbu sawa mbele ya mkutano na waandishi wa habari, baada ya kuwepo taarifa za upotoshaji kuwa yuko Mjini Dodoma kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba Mpya vinavyoendelea mjini humo.

"Hizi ni mbinu za kitoto za kutaka kuniharibia jina langu na kazi zangu za kisiasa. Mimi Chiku Abwao nitakuwa mmoja wa watu wa mwisho kabisa kukisaliti chama changu...nitakuwa mmoja wa watu wa mwisho kabisa kusaliti mageuzi na mabadiliko ya mfumo na utaawala ambayo nimeyapigania sehemu kubwa ya maisha yangu.

"Natambua msimamo wa kuwataka wabunge na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na chama chetu kutohudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba Mpya ni azimio la Kamati Kuu ya Chama ambayo mimi pia ni mjumbe, siwezi kukiuka maagizo ya chama.

"Chama kupitia Kamati Kuu kiliazimia kwamba wajumbe wanaotokana na CHADEMA tutaungana na wenzetu wengine kwenye UKAWA kutohudhuria vikao vya Bunge Maalum kwa sababu hakuna nia ya dhati ya kutafuta maridhiano ya kitaifa katika mchakato huu kwa kujadili maoni ya wananchi bungeni.

"Mimi siwezi kuja hapa Dodoma kusaliti UKAWA na kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba...maamuzi ya UKAWA ni maamuzi ya wananchi, siwezi kuja hapa kuwasaliti wananchi. Ninajua ninachokifanya katika siasa za mageuzi, ni kutumikia wananchi si kutafuta maslahi," amesema Abwao.

Abwao amezidi kufafanua kwamba aliwasili Dodoma kwa ajili ya kuchukua gari yake aliyoiacha katika yard ya bunge wakati alipoondoka nchini kwenda Australia akiwa sehemu ya ujumbe wa Bunge, kuiwakilisha nchi kwenye mkutano wa masuala ya UKIMWI.

Amesema kuwa alipofika mjini Dodoma alikwenda kulichukua gari lake kwenye yard ya bunge (viunga vya bunge) na akaanza kulifanyia matengenezo kwa ajili ya safari ya kwenda Iringa.

"Siku ya jana (Jumatano) nimekuwa na kazi ya kuzunguka hapa mjini kutafuta spares kwa ajili ya kutengeneza gari langu...sasa nimeonekana sana huko kwa sababu nilikuwa natumia usafiri wa taksi...wao wakaamua kufanya propaganda za kwamba mimi niko hapa kuhudhuria Bunge Maalum. Wanapoteza muda wao. Tuko na wananchi," amesema Abwao.

Saturday, July 19, 2014

TASWIRA : KAMATI KUU YA CHADEMA YAKUTANA DAR


TAMKO KUHUSU KUONDOKA KWA WALIOKUWA VIONGOZI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kigoma Kaskazini tunapenda kutoa taarifa kwa umma kutokana na sintofahamu inayotaka kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu uimara wa chama chetu mkoani Kigoma.
Tangu jana na leo kumeenea taarifa zinazowahusu watu watatu, Jaffari Kasisiko, Msafiri Wamarwa na Mama Malunga Masoud, ambao vyombo mbalimbali vya habari vimeandika kuwa wamehama chama chetu cha CHADEMA na kukimbilia wanakojua wao (maana CCM inafanya kazi zake katika sura mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;

1. Kwanza watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama ngazi ya mkoa, kwa uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi cha muda mrefu sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika mkoa mzima wa Kigoma ili kiweze kukimbizana na wenzetu wa maeneo mengine nchi nzima. Badala yake walikikumbatia na kukiatamia chama. Wakati maeneo mengine wenzetu wakiongeza wabunge majimboni, Kigoma chini ya uongozi wao ikauza majimbo.

2. Tunaweza kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako mbioni kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa ni sawa na KOTI LILILOTUBANA. Kwa muda wao wote wa uongozi hawakuwahi kufanya kazi yoyote ya kioganazesheni na kukieneza chama mkoa mzima. Wao walikuwa watu wa mikutano ya hapa na pale Kigoma mjini pekee au pale ambapo kunakuwa na uongozi wa kitaifa au wabunge.

3. Kwa muda mrefu saa wamekuwa viongozi ‘waliotubana’ kwa sababu walifanya kazi kwa kuangalia zaidi maslahi yao. Sasa kuondoka kwao, ni nafuu kwa chama. Pia ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa wanachama makamanda waaminifu na watiifu waliofungiwa milango kwa muda mrefu, kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa imani kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge.

4. Upo ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi hao na wengine wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, wamekuwa wakilalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na maelekezo ya CCM.

5. Katika madai yao ya kuhama chama watu hao wamesema wamefikia hatua hiyo eti kutokana na chama chetu kuwa cha kibabe eti kwa sababu tu Zitto Kabwe alivuliwa nafasi Naibu Katibu Mkuu ndani ya chama!

6. Madai hayo yanashangaza kwa sababu mbali ya chama kuwa na sababu nzito za kumvua Zitto (na wenzake akina Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) cheo hicho kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu, pia tunaamini hakuna mwanaCHADEMA amejiunga na chama hiki kwa ajili ya cheo. Ndani ya chama chetu tunaamini katika kugawana majukumu si vyeo.

7. Katika hali ya kushangaza zaidi wanasema eti Zitto amezuiwa kugombea uenyekiti. Sasa tunajiuliza hiyo nia ya kugombea ambayo hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na itifaki za chama, waliambizana wao wenyewe na mtu wao? Lakini kwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari Kasisiko analipa fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya nchi.

8. Ninaomba kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa wilaya na majimbo ya Kasulu Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini, tukutane kwa ajili ya kikao cha Baraza la Mashauriano la Mkoa ili sasa tuchukue hatua zingine za muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha chama chetu kwa kuwaondoa vibaraka na wasaliti wote waliosalia.

9. Pia tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia kiingilie kwa kutumia kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha kuendelea kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua hiyo kupitia Baraza la Mashauriano.

10. Sisi wa CHADEMA Kigoma Kaskazini tunawataka wale wengine waliosalia katika mkakati huo wa kuhamisha watu wachache lakini kwa makundi ili eti kujenga taswira ya CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi kadhaa wa Kanda wasisubiri. Chama chetu kitajengwa na watu wenye imani watakaoweka maslahi na matakwa ya wananchi mbele kwa kuzingatia misingi yetu kama inavyoelezwa katika Katiba ya Chama, kanuni, maadili na miongozo.

Kwa niaba ya Wanachadema imara na makamanda watiifu na waaminifu kwa mabadiliko yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge, naomba kutoa taarifa hii.

Ally Kisala
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma